Habari

Sababu za shirika la Ndege la Kenya kusitisha safari zake Uingereza (+ Video)

Shirika la Ndege la Kenya, Kenya Airways (KQ) limetangaza kwamba litasitisha safari za kwenda na kuondoka nchini Uingereza kuanzia Ijumaa tarehe 9 mwezi huu .

Uamuzi huo umechukuliwa kufuatia agizo la serikali ya Kenya kuzuia safari zote za ndege kati ya nchi hizo mbili kuanzia siku hiyo.

KQ kupitia taarifa imesema imezidisha ndege mbili Zaidi kufanya ziara kati ya nchi hizo mbili tarehe 7 na tarehe 8 mwezi huu .KQ imewashauri wateja wake waliokuwa wamekata tiketi za kusafiri kubadilisha tarehe zao za kusafiri au watoe ombi la kurejeshewa fedha walizokuwa wamelipa kama nauli . Tiketi zote zinafaa kutumika kufikia tarehe 31 Machi mwaka wa 2022 .

Kenya iliamua kujibu marufuku ya Uingereza kwa kuwawekea raia wa nchi hiyo watakaowasili sharti la kuwa karantini kwa siku 14.

Raia wa Uingereza watakapokuwa wamejitenga, watahitajika kupimwa ikiwa wamepata maambukizi ya virusi vya corona au la mara mbili siku ya pili na ya nane wakiwa karantini kwa gharama zao wenyewe.

Pia katika taarifa hiyo iliyotolewa Jumamosi, ilisema kuwa masharti hayo yanaanza kutekelezwa saa sita usiku wa Aprili 9, 2021.

 

Hata hivyo, ndege za kubeba mizigo kati ya nchi hizo mbili zitaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia masharti mengine yatakayotangazwa.

Aidha, raia wa Kenya wanaoishi Uingereza au watakaopitia viwanja vya ndege vya Uingereza kuingia Kenya hawataguswa na masharti hayo mapya.

Hatua ya Kenya imewadia baada ya Uingereza kufanya maamuzi ya kuijumuisha Kenya kwenye orodha ya watakaopigwa marufuku kuingia nchini humo kama njia moja ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Wizara ya mambo ya nje ya Kenya ilisema kwamba hatua iliyochukuliwa na Uingereza inatatiza hasa baada ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

“Uamuzi uliochukuliwa na Uingereza utaathiri Kenya kwa kiasi kikubwa hasa kibiashara kati ya Kenya na Uingereza, usafiri, utalii na ushirikiano wa kiusalama,” Wizara ilisema.

Uhuru Kenyatta na Boris Johnson

Pia wizara ya Kenya ilisistiza kuwa hatua ya uamuzi huo utatatiza shughuli za nchi hizo mbili hasa ikizingatiwa kwamba zimekuwa na ushirikiano wa nyanja mbalimbali kama vile afya, elimu na hata baina ya watu.

“Zaidi, uamuzi huo wa upande mmoja haukuakisi mantiki na ufahamu wa kisayansi kuhusu ugonjwa huo au kusambaa kwa janga. Badala yake unaonekana kuchochewa na sera ya kubaguzi dhidi ya mataifa mengine na watu wake”.

Serikali ya Kenya pia ilizungumzia kusikitishwa na kile ilicho kiita ubaguzi wa chanjo ambapo nchi zinazotengeneza chanjo sasa zinabagua nchi zingine na kuamua kijiwekea akiba.

“Kenya bado imesalia na maoni yake kwamba serikali ya Uingereza ingeiunga mkono kwa kuipatia chanjo. Hii ni baada ya Kenya kuiomba Uingereza kuigawanya chanjo zake ambayo inafahamu kwamba ina idadi kubwa kuliko zile inazotumia kwa sasa”.

Wizara ya mambo ya nje iliongeza kuwa wimbi la tatu la maambukizi ambalo Kenya inakabiliana nalo sasa hivi na hatua ilizochukua, ni mfano vile Wakenya walivyojitolea kuhakikisha ugonjwa wa corona hausambai ama nchini Kenya au kwingineko duniani.

Pia Kenya imezungumzia ufahamu kwa kwamba chimbuko la ugonjwa huo sio Afrika, hauna mipaka na wala haujakuwepo kwa muda mrefu kwa mwanadamu kuweza kuelewa mabadiliko ya siku za usoni.

Bofya hapa chini kutazama.

https://www.instagram.com/tv/CNUOZXMB648/

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents