Habari

Siku 12, Trump kukabidhi Ikulu kwa Joe Biden

Hatimae Rais Trump awalaani waliovamia bunge na kufanya fujo. Huku zikiwa zimebaki siku 12 kabla ya kumalizika kipindi chake cha uongozi na kuapishwa rais mteule Joe Biden ifikapo Januari 20,2021, Rais huyo pia amekiri kwamba ataondoka kwa amani baada ya bunge kuthibitisha kushindwa kwake.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema amekasirishwa na watu hao ambao ni wafuasi wake waliotumia nguvu na kufanya vurugu ndani ya ofisi za bunge baada ya kulivamia. Trump amesema watu hao waliyahujumu makao makuu ya demokrasia ya nchini Marekani na ameeleza kuwa waliofanya vurugu hizo wanapaswa kulaaniwa na kuadhibiwa.

Rais Donald Trump kwa mara ya kwanza amekiri kwamba Joe Biden ni rais ajae wa Marekani, ametamka hayo siku moja baada ya wafuasi wake kuvamia bunge wakati lilipokuwa linajiandaa kuthibitisha ushindi wa Biden. Trump amesema la muhimu sasa ni kuhakikisha kuwa zoezi la kubadilishana madaraka linakwenda vizuri.

Kauli hiyo imeonesha ugeugeu wa Trump tofauti na Trump yule aliyetumia miezi kadhaa akisisitiza kuwa alishindwa kwenye uchaguzi wa Novemba 3 kutokana na udanganyifu uliotokea, bila ya kutoa ushahidi. Trump ametoa matamshi hayo baada ya wabunge wa vyama vyote viwili pamoja na viongozi waandamizi katika utawala wa rais huyo kuanza mazungumzo juu ya kumwondoa madarakani.

Spika wa Bunge la Marekani Nancy PelosiSpika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi

Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema ikiwa hataondolewa kwa njia ya kutumia ibara ya 25 ya katiba ya Marekani basi bunge litajaribu kwa mara ya pili kumfungulia mashtaka juu ya kumwondoa madarakani. Spika Pelosi moja kwa moja amemlaumu rais Trump kwa kuchochea alichoita uasi wa kutumia nguvu dhidi ya Marekani.

Spika Pelosi na kiongozi wa maseneta wa chama cha Democrats Chuck Schumer walijaribu kuwasiliana kwa njia ya simu na makamu wa rais Mike Pence kumtaka achukue nafasi ya rais Trump mara moja kwa mujibu wa kipengele hicho cha 25 cha katiba ya Marekani kinachomruhusu makamu wa rais kuchukua hatua hiyo, ikiwa rais ameshindwa kuyatimiza majukumu yake.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents