Habari

Simu za mkononi, janga jipya ajali za barabarani

NA JANETH JOVIN

TEKNOLOJIA ni elimu au maarifa yanayohusu uhandisi, ufundi, ujenzi na mbinu za uzalishaji wa vifaa na huduma katika jamii.

Asili ya neno hili ni lugha ya Kigiriki, ikimaanisha uwezo, usanii na ufundi kama vile wa vifaa na mashine zinazotumika katika uundaji wa kitu na matengenezo au uzalishaji wa vitu.

Mbali ya uundaji wake, pia unahusisha elimu ya matumizi yake pamoja na mbinu na maarifa jinsi ya kutumia sayansi. Aidha, ni uwezo wa kubadili malighafi asilia na kuwa bidhaa yenye thamani inayoweza kukidhi mahitaji ya binadamu.

Hapa bidhaa haimaanishi tu vitu kama magodoro, magari ya kutembelea, unga wa ngano na kadhalika, ni huduma yoyote inayotolewa kwa jamii.

Kwa mfano, huduma ya usafiri, huduma ya utalii, huduma ya chakula, na pamoja na vitu vyote vinavyozalishwa viwandani.

Teknolojia nyepesi kabisa ni ujuzi wa kutumia vyombo katika hali ya kurahisisha kazi katika kuyafikia mafanikio na maendeleo kwa njia rahisi.

Kwa mfano, katika somo la historia, mwanadamu alivumbua teknolojia ya kuwasha na kudhibiti moto ambao ulimwezesha kupika.

Pia, aliweza kutumia mawe kwa kulima na kuwinda. Kadri wakati ulivyoenda ndivyo teknolojia yake ilivyoboreshwa kwa mfano kwa uvumbuzi wa gurudumu lililorahisisha ukulima na kusafiri kwake.

Maendeleo ya teknolojia ya kale yalihusisha zaidi uvumbuzi wa chombo cha kupiga chapa, simu na mtandao ambazo zimefanya mawasiliano yawe rahisi.

Hata katika udhibiti wa ajali za barabarani, kumekuwepo na teknolojia zinatumika, japo ni matokeo ya makosa ya kibinadamu, ubovu wa barabara na vyombo vya moto hata sababu za kimazingira.

Kwa upande wa mwendokasi, ni mojawapo ya visababishi vitano vya ajali za barabarani, chanzo kikubwa makosa ya uzembe wa madereva.

Takwimu za ajali nchini zinaonesha, kisababishi kingine cha ajali za barabarani, ni matumizi ya simu ambayo huwafanya madereva wengi kukosa umakini na kujikuta wakiendesha kwa mwendokasi.

Kumbe, pamoja na faida ya teknolojia ya mawasiliano ya simu katika maendeleo ya mwanadamu, pia simu kwa sasa ni janga kubwa linalokatisha uhai wa wengi na kuchangia utokeaji wa ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuna ongezeko la watumiaji wa simu hizo za mkononi.

Hivyo, ongezeko hilo la watumiaji wa simu za mkononi, limeteka akili za baadhi ya watumiaji kiasi cha kuendesha hovyo vyombo vya moto na kujikuta wakigongwa na gari au pikipiki wakati wa kuvuka barabara huku wakitumia simu.

Simu za mkononi zimekuwa zikichangia ajali nchini kutokana na dereva wa vyombo vya moto kuendesha gari wakati akitumia simu iwe kusikiliza, kuzungumza ama kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms).

Sababu nyingine ni wengine kuangalia picha mbali mbali kutoka katika mitandao ya simu, jambo ambalo linamfanya umakini barabarani upungue.

Kwa mujibu wa Ripoti ya takwimu za TCRA ya robo ya pili ya mwaka 2023 (Aprili hadi Juni 2023) imebainisha kuwa watumiaji wameongezeka kutoka milioni 61.9 walioripotiwa Machi 2023 hadi kufikia milioni 64.1 mwaka ulioishia Juni 2023.

Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 3.6 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Idadi ya watumiaji wa simu imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja unaoishia Juni 2023, watumiaji wa vifaa hivyo vya mawasiliano wameongezeka kutoka milioni 56.2 walioripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

Kimataifa, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ripoti yake ya usalama barabarani ya mwaka 2018, zinaonyesha zaidi ya watu Milioni 1.3 hufariki dunia kila mwaka kwa ajali za barabarani duniani kote.

Aidha, WHO katika ripoti hiyo ilieleza kila sekunde 24 duniani, mtu mmoja hupoteza maisha kwa ajali za barabarani na ifikapo mwaka 2030, wataongezena na kufikia Milioni 1.9, iwapo hatua za kudhibiti vifo hivyo hazitachukuliwa.

Hata hivyo, matumizi ya simu yanatajwa kuwa ni miongoni mwa makosa yanayochangia kutokea kwa ajali hizo zinazokatisha maisha ya watu.

Pia, ripoti hiyo inasema utumiaji wa simu wakati wa kuendesha ikiwa imeshikwa mkononi au bila kushika, kuna uwezekano wa kusababisha ajali mara nne huku kuendesha ukiwa unatuma au kusoma ujumbe mfupi wa maneno (message) kunakuweka kwenye hatari ya kupata ajali mara 23.

Kwamba, Tanzania haijaweka sheria madhubuti kudhibiti matumizi ya simu za mkononi barabarani ikilinganishwa na nchi zingine za Afrika Mashariki hususani Kenya na Uganda ambazo tayari zinasheria hiyo.

Mwenyekiti wa Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), John Seka anasema sheria ya Usalama Barabarani ya Tanzania haina kifungu wala kipengele chochote kinachopiga marufuku matumizi ya simu za mkononi wakati wa kuendesha gari na kusema kuwa hayo ndio mapufungu yaliyopo.

Anasema ila kwa sasa mtu anaweza kushtakiwa kwa kifungu namba 42 kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe na hatari endapo matumizi ya hivyo vifaa yalisabaisha ajali.

“Mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yanajaribu kuingiza kosa hili kama kifungu kitakachojitemea,” anasema Seka.

Seka anasema kwa mujibu wa kanuni mpya za usafirishaji wa abiria za mwaka 2017 za Latra, hakuna kifungu kinachokataza matumzi ya simu kwa dereva.

“Ila kanuni za usafirishaji mizigo za 2012 katika kifungu cha 28 (h) zimeweka katazo la matumizi ya simu, kanuni hizi zinasomwa pamoja na zile za 2017,” anasema

Aidha anasema matumizi ya simu na vifaa vya eletroniki vinamfanya dereva kukosa umakini anapokuwa barabarani hivyo ni muhimu kwa sheria kuwa na kifungu cha kuweka katazo la vitu hivyo wakati wa kuendesha au kutumia chombo cha moto ili kupunguza ajali.

“Hivyo kama tutafanikiwa kurekebisha sheria na kupiga marufuku matumizi ya simu wakati wa kuendesha na watu wakatii sheria bila shuruti basi tutakuwa tumepunguza idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani,” anasema

Naye aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Kikosi cha Usalama barabarani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Deus Sokoni anasisitiza kuwa katika mapendekezo ya sheria ya usalama barabarani ambayo mpaka sasa haijulikani kama yatapitishwa, matumizi ya simu wakati dereva anaendesha gari yalipigwa marufuku.

Anasema madhara ya simu ni makubwa na ndiyo maana serikali imeamua kwamba kwenye sheria mpya ihakikishe inaingiza marufuku ya dereva kutumia simu ili kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

“Yaani marufuku itakuwa ni kwa dereva kushika simu kwa madhumuni ya kupiga au kuandika ujumbe mfupi wa maneno wakati anaendesha gari,”anasema Sokoni.

Anasisitiza kuwa simu zina madhara makubwa kwani wakati mwingine dereva anaperuzi mitandao ya kijamii au kuangalia picha kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo ni hatari kubwa.

“Matumizi haya ya simu yanachangia dereva kuendesha gari kwa mwendo kasi maana unamkuta mtu yupo bize anaangalia video huku anajisahau hata ameweka speed ngapi katika gari,” anasema

Anasema kwa sasa sheria ya usalama barabarani haizungumzii lolote kuhusu matumizi ya simu na ndiyo maana Polisi wa usalama barabarani hawakamati mtu ambaye anazungumza na simu kwa sababu hakuna sheria ya kumbana.

Maazimio

Mei 23, mwaka 2021, Katika Kongamano la usalama barabarani liliofanyika Bungeni Dodoma katika ukumbi wa Puis Msekwa moja ya maazimio yaliyofanyika katika suala la mwendo kasi ni kuboresha kifungu cha sheria 51 (8) cha usalama barabarani.

Kongamano hilo limependekeza kuwa kiwango cha mwendo kasi kinapaswa kupunguza na kuwa Km 50 kwa saa kwa maeneo ya mjini na makazi na Km 30 kwa saa kwenye maeneo ya shuleni, masoko na kwenye alama ya waenda kwa miguu na wanyama.

Pia, kuongeza kifungu kinachofafanua na kuainisha maeneo ya makazi ni yapi.

Hata hivyo hadi leo tunapozungumza hakuna sheria mpya ya usalama barabarani ambayo ilikuwa kipigiwa kelele kwa muda mrefu na wadau mbalimbali.

Wadau wa usalama wa barabarani nchini wametaja kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa upande wa Serikali kama sababu kuu ya Tanzania kushindwa kuwa na sheria mpya na ya kisasa ya usalama barabarani ambayo wanaamini ingesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza ajali za barabarani nchini.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani wa mwaka 2021 ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni mnamo Juni 30, 2021, ikiwa ni baada ya miaka takriban sita ya ushawishi, uchechemuzi na vuguvugu kufanikisha hatua hiyo. Hata hivyo, tangu kusomwa kwake muswada huo ulipotolea kusikojulikana na hivyo hatma yake kutojulikana.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents