Habari

Waziri Mkuu aitaka Wizara ya Maliasili kutafuta mbinu bora za kutangaza vivutio

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kutafuta mbinu bora za kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ili kukuza sekta hiyo.

Waziri Mkuu aliyasema hayo wakati alipofanya ziara katika mji wa kitalii wa Varadero ulioko kwenye mkoa wa Matanzas nchini Cuba.

Alisema mji wa Varadero tu unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa kilomita 22.

Aidha alisema idadi hiyo ni tofauti na Tanzania ambayo imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku watalii wanaovitembelea ni wachache. “Tunatakiwa kujitangaza zaidi.” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alitaja baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo ni mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, miji ya kihistoria ya Kilwa, Bagamoyo, Stone Town pamoja na Mikindani.

“Vivutio vingine ni eneo la Oldvai George ambako binadamu wa kwanza aliwahi kuishi, hifadhi ya Gombe ambako kuna sokwe ambao wanaishi kama binadamu.”

Hata hivyo alisema Serikali itahakikisha jitihada zinafanyika katika kukuza sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vilivyoko nchini ili kuweza kuongeza idadi ya watalii.

Pia Waziri Mkuu aliwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kutembelea vivutio vyeo vya utalii na kujifunza mambo mbalimbali na si kuwaachia wageni pekee.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Sekta ya Utalii katika mkoa wa Matanzas, Bw. Luis Martinez de Armas alisema mji wa Varadero ni kivutio kikubwa cha utalii nchini Cuba.

Hata hivyo Bw. Luis alisema Tanzania inavivutio vingi vya utalii na kwamba anavutiwa na mlima Kilimanjaro pamoja na wanyama na viumbe vingine vilivyoko katika mbuga mbalimbali. Alisema wako tayari kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya utalii.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents