Burudani

Alipokuwa kwenye ubora wake: Nyimbo 10 kali alizoshirikishwa Chidi Benz

Wakati fulani ingekuwa ni dhambi kubwa kuwataja rappers bora bongo bila kumweka Rashid Makwiro kwenye orodha hiyo. Kila alichogusa kwa wakati ule kiligeuka dhahabu kila wimbo uliobahatika kuwa na sauti yake ulikuwa na uhakika unakwenda kuwa hit kwenye radio station.

148924_377053065678142_419058462_n

Ungekuwa umewachokoza ‘raia wema’ na ingekuchukua muda mrefu kukuelewa kama Rashid asingebeba tuzo kwenye Kilimanjaro Music Awards. Zilikuwa tuzo zake wakati ule tena bila wasiwasi wowote.
Maisha yamebadilika hayupo pale alipotakiwa kuwa Chidi Benz huyu sio yule mtoto wa Ilala aliweza kuwakusanya wakina Tunda Man,Ditto na Cassim Mganga kuunda moja kati ya makundi bora kuwahi kutokea kwenye bongo flava, La Familia.

Pengine matumizi ya dawa za kulevya ndio kikwazo chake kikuu huku ishu ya kukamatwa na kete kadhaa kwenye mfuko wa shati lake pale Mwalimu Nyerere International Airport ikimpeleka chini zaidi. Ila inatia faraja kusikia ameacha hizo kitu na kuamua kuwekeza nguvu zake tena kwenye muziki kama zamani.

Nakuleta orodha ya nyimbo 10 kali ambazo zilipendeza zikiwa na sauti nzito ya rapper huyu wa Ilala maghorofani

Neila – Tundaman

https://www.youtube.com/watch?v=JNi2O2XXiss

Tunda man kwenye ubora wake alifanya jambo jema mno kumweka “kaka yake” kwenye wimbo huu. Wimbo mkali wa mapenzi ulianzisha safari njema kwenye maisha ya mziki ya Tunda na popote alipo Tunda ameendelea kumshukuru Chidi Benz kwa kukubali kumsadia wakati ule.
“Story maskani hazipandi kama mtoro na masomo” anasikika aki-rap Rashid kwenye wimbo huo.

Hao – Mwasiti

https://www.youtube.com/watch?v=b6AqcxsxNY0

Mwasiti na Chidi, producer Lamar alitengeneza moja kati ya beat bora kuwahi kutengeneza na bahati nzuri beat ile ilidondokea kwenye “mikono salama” ya Chidi Benz na kuipeleka sehemu nyingine kubwa zaidi.

Baada ya wimbo huu kila mtu alimjua vyema zaidi Mwasiti na pengine huu waweza kuwa wimbo bora zaidi kutoka kwake. ‘Wanoknok wakusema mabaya,wana talk talk mdomoni wanatema fire,’ Chidi anasikika akiunguruma kwa hisia kwenye wimbo huu.

Bado Umenuna – Marlaw

Moja kati ya nyimbo bora zaidi kuwahi kutokea kwenye Bongo flava. Wimbo huu ulijikusanyia tuzo kadhaa kwenye Kilimanjaro Music Awards na ulimpa thamani kubwa zaidi Chidi Benz kwa tabia yake kinyonga kuweza ku-rap kwenye kila aina ya beat kwa uwezo ule ule.

Ni wimbo mzuri wa mapenzi jamaa akijaribu kumbeleza mpenzi wake asinune zaidi na kukubali wayamalize matatizo yao. ‘Njoo nipige hata makofi nitatii amri mi kiraka wewe ndo boss,’ anarap Chidi kwenye moja ya mistari ya wimbo huu.

Usiniache – Spack

https://www.youtube.com/watch?v=fHukDKiD_1M

Kutoka Ilala mpaka Manzese, Spack wa Tip Top Connection alifanya moja kati ya jambo jema kwenye maisha yake ya kimuziki.

Ulikuwa wimbo fulani unamhusu ‘mchizi’ aliyegombana na mpenzi wake na msichana kuamua kurudi kwao huku akiacha ujumbe wa kipande cha karatasi.Mchizi anarudi toka misele yake anakuta ujumbe juu ya meza huku mpenzi wake akiwa hayupo.

Anafunga safari mpaka ‘ukweni’ kwenda kumpigia magoti mpenzi wake na kwa bahati nzuri ‘mshkaji’ wake Chidi Benz anaweka maneno yake mazuri ya kimapenzi kumrudisha tena yule msichana kwenye himaya ya Spark.

‘Utakuwa kama umeng’oa kiraka kwenye jeans ya bishoo tena bishoo matata,’ Chid anajaribu kumbeleza kwa maneno matamu yule binti.

Tell Me Why – Makamua

Makamua akiwa kwenye ubora wake. Ungesema nini zaidi kuhusu uwezo wa kuimba kwa hisia aliokuwa nao Makamua.
Kwa watu wengi huyu ni mmoja kati ya wasanii bora wa Rnb waliowahi kutokea Tanzania.

Bahati mbaya wapo wachache wa aina yake ukimuondoa Ben Pol,Rama Dee,Belle 9 na Jux utapata tabu kuwatafuta wengine wa aina yake.
Akiwa anatokea Kundi la Wakali Kwanza na washkaji zake, QJ na Joslin walijua nini cha kufanya kuiteka Bongo Flava na kuiweka upande wao.Bahati nzuri mkali yule wa Rnb alikutana na mkali wa Hip Hop na kufanya moja kati ya nyimbo bora ya mapenzi ya muda wote.

‘Kidume nalia haya yote sababu yako, Mungu alijalia akanipa uwe wangu nashangaa leo sikuoni tena kipenzi change,’ Chid anasika aki-rap kwenye beat tamu ya gitaa.

Heshima – Geez Mabovu

Geez Mabovu aliwakusanya Jay Moe,Fid Q na Chidi Beenz kuitengeneza ngoma hii kali pale kwa Lamar. Ni wimbo fulani mkubwa ambao ndani yake kuna mambo mengi makubwa kutoka kwa watu wakubwa.

‘MC mdogo kiumbo ila mkubwa kisauti ona waliojaa matumbo wanavyonipigia saluti,’ ni moja kati ya mistari ya kibabe ya Chidi kwenye wimbo huo.

Ninaposimama – Langa

Langa(R.I.P) aliamua kufanya jambo la heri kumweka Chidi kwenye wimbo huu. Nadhani ukiondoa wimbo wa Matawi ya Juu, huu ni wimbo bora zaidi kutoka kwa Langa na bahati nzuri wimbo huu ulimkuta Chidi akiwa kwenye ubora na hakutaka aushushe ubora wake.

Kilichotokea ni wimbo mmoja mkali wa Hip Hop utakaobaki kwenye vichwa vya watu wengi kwa muda mrefu.

‘Nafuta vumbi kila baada ya saa,wanasema mi bishoo yeah bishoo haswa,’ ni moja kati ya mistari mikali kutoka kwa Chidi Benz kwenye wimbo huu ambayo ilimvutia pia Quick Rocka kuitumia kwenye wimbo wake Bishoo.

Nihurumie – Ray C

Ray C kwenye ubora wake. Wakati ule kila msanii mkali angetamani kufanya wimbo mkali na Ray C.Hatuzungumzii kuhusu kiuno chake bila mfupa, lahashaa, ni uwezo wake mkubwa wa kuimba kwa hisia.
Chidi Beenz alitokea kama mtende jangwani kwenye wimbo ule na kuufanya uwe wimbo mmoja kati wimbo mkali wa kimapenzi kama kawaida ya Ray C.

‘Amini siwezi kudata na wa mjini,mpaka milele sikuachi mimi na wewe kama kidevu na mustache,’ anasikika Chidi akimbembeleza mtoto wa kike.

Speed 120 – Ngwair

Mwaka 2003 wakati ule kila mtu akimjua Albert Mangwea(rip) kama rapper bora, alikutana na Chidi anaetafuta kutoka pale Club Bilicanas. Ngwea akiwa kama mfalme wa free style huku Chidi akiwa mfalme wa freestyle pale mtaani kwake Ilala.

Wakawekwa jukwaani na kila mmoja akidondosha free style za hatari mwisho wa siku hakutangazwa mshindi ni nani , iliachwa kila shabiki abaki na jibu lake mwenyewe.

Kitu kile kiliangaza mwanga mwema kwa Chidi aliyekuwa anatafuta njia za kwenda kuwa staa na bahati nzuri kwake usiku ule ulizalisha urafiki mzuri kati yake na Ngwea na kwenda kutengeneza wimbo pamoja wimbo uliotwa, ‘Wakati Ndio Huu’ ila bahati mbaya haukupenya vya kutosha kwa watu wengi.

Baada ya miaka mingi wakati huo kila mtu akiwa staa wa Hip Hop, wakaja kufanya ngoma nyingine. Safari hii Ngwea akimshirisha Chid. Speed 120 ilikuwa jina la wimbo na kama jina lake lilivyo wimbo ulitamba kwa speed ile pia.

‘Life langu lipo simple ndio maana naweza vaa suti nikanukia majani,’ anasikia Chidi aki-rap.

Nalia na Mengi – Diamond Platnumz

Mwaka 2008 Chidi Benz akiwa kwenye ubora wake alipigiwa simu na mshkaji mmoja hivi asiyemjua aliyeomba amshirikishe kwenye wimbo wake. Chidi hakuwa anamjua yule mshkaji ila akamwambia aende Ilala.

Baada ya masaa kadhaa mshkaji mmoja hivi mwembamba mrefu alionekana akitokea maskani ya La Familia. Baada maongezi ya dakika kadhaa kati ya Chidi na yule dogo mwembamba,Chidi alimwambia yule dogo ‘nakusaidia bure hutonipa hata senti moja kwa sababu wewe ni jasiri na pia utafika mbali mno una nuru ya mafanikio kwenye uso wako.’

Walifunga safari ya pamoja mpaka studio kwenda kufanya wimbo mmoja kati ya nyimbo nzuri za yule dogo. Yule dogo alikuwa ni Diamond Platnumz ambaye leo amekuwa staa wa Afrika nzima!

Nalia na Mengi ilikuwa jina la wimbo wa Diamond akiwa amemshirikisha Chidi Benz. Ni moja kati ya nyimbo zilizofungua njia nzuri ya mafanikio kwa Diamond pengine bila ujasiri wa Diamond kwenda kuonana na Chidi asingefika hapa alipo.

‘Nitakulinda kama mkinga mwenye shamba, usiombe mapenzi yakupige teke yanauma,’ Chidi anachana.

Makala hii imeandikwa na Heri Best: Unaweza kumfollow Instagram kwa jina @heri_best na Twitter, @mimi_Heri. Makala imehaririwa na Fredrick Bundala (Twitter na Instagram: @skytanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents