Michezo

Benki ya NMB yajitosa kwenye udhamini wa Bima Marathon 2020

Benki ya NMB yajitosa kwenye udhamini wa Bima Marathon 2020

Benki ya NMB, imetangazwa kuwa Mdhamini Mkuu wa Mbio za Bima Marathon 2020, zinazotarajiwa kufanyika Machi 28 jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Kampuni ya African Digital Banking Summit.  Kwa udhamini huo, mbio hizo zinazoenda kufanyika kwa mara ya pili mfululizo, zitatambulika kwa jina la NMB Bima Marathon 2020, ambazo zitahusisha mbio za kilomita 21, kilomita 10 na kilomita tano.

NMB imedhamini mbio hizo kwa kitita cha Sh. Milioni 35, ambako hafla ya NMB kutangaza udhamini wake huo katika mashindano hayo imefanyika jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi ya udhamini, Meneja Mwandamizi wa Bima wa NMB, Martine Massawe, alisema wamevutiwa kudhamini Bima Marathon kutokana na mlengo wake.

“Mashindano haya yanatumika kama jukwaa la kutoa elimu ya Bima kwa Watanzania, lakini pia kuimarisha afya. Nasi tumeona ni fursa tunayoweza kuitumia kutangaza huduma mpya ya Bancassuarance. Lakini hii sio mara ya kwanza kwetu NMB kudhamini michezo, tumefanya hivyo katika soka ambako tumeidhamini Taifa Stars na timu za Azam FC na Singida United. Tumefanya hivyo pia katika mpira wa magongo, gofu na kriketi na kadhalika,” alisema Massawe.

Alitumia fursa hiyo kuwatakia Watanzania kujenga utamaduni chanya wa kutumia bima kadri ya matahitaji yao, kwa kutembelea matawi yote 224 kote nchini na kukata bima mbalimbali zikiwamo za maisha, magari, afya, nyumba, kilimo na dhamana kutoka kwa wabia wake.

Meneja Mwandamizi wa Bima NMB Martine Massawe (kulia) akikabidhi mfano wa hundi ya Sh milioni 35 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa African Digital Banking Summit Limited – Baraka Mtavangu kwa ajili ya NMB Bima Marathon zitazofanyika tarehe 28 mwezi wa tatu jijini Dar es Salaam. Katikati ni Meneja wa NMB Jogging Club, Elifadhili Mramba.

Huduma za bima zitakazopatikana katika matawi ya NMB ni pamoja na zile za Kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Jubilee Insurance, Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) na Reliance Insurance.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya African Digital Banking Summit inayoratibu mbio hizo, Baraka Mtavangu, aliipongeza NMB kwa udhamini, anaoamini unaenda kubadili taswira ya mashindano hayo.

Alibainisha kuwa, mbio hizo zitanatarajia kushirikisha wakimbiaji watu wazima wapatao 3,500 na watoto 500, na kwamba usajili unafanyika katika vituo mbalimbali, ikiwemo Mlimani city na baadhi ya matawi ya NMB kwa Sh. 20,000 kwa watu wazima na Sh. 15,000 kwa watoto.

Kutakuwa na Washindi wa kwanza hadi wa tano katika mbio za kilomita 21 na kilomita 10, ambako mshindi wa km 21 atatwaa Sh. Mil. 1, huku mshindi wa km 10 atajishindia Sh. 700,000. Zawadi zingine zitatangazwa baadaye,” alisema Mtavangu.

Mratibu huyo alilishukuru Shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT) kwa sapoti, ushirikiano na kibali cha uendeshaji wa mbio hizo, ambazo alisema zitashirikisha Watanzania na wageni wanaoishi nchini, huku wakimbiaji wa nje wakitakiwa kujiandikisha kupitia chama cha riadha nchini.

#Umebima?

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents