Habari

Breaking: Mtikila ashinda kesi ya uchochezi

MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameshinda kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili.


Inadaiwa kuwa Oktoba 21 mwaka jana katika maeneo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Ilala, jijini Dar es Salaam Mchungaji Mtikila alitoa maneno ya uchochezi, dharau na kujenga chuki dhidi ya Serikali na Rais.

Mchungaji Mtikila aliwasili mahakamani hapo majira ya saa 4 asubuhi ambapo hukumu ya kesI yake ilianza kusomwa majira ya saa 6 mchana kwa muda wa nusu saa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Ilvin Mgeta.

Hakimu Mgeta amesema amelazimika kumwachia huru Mchungaji Christopher Mtikila baada ya upande wa jamuhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka hayo.

Mchungaji Mtikila anadaiwa kati ya januari mwaka 2009 na aprili 17 mwaka 2010 jijini Dar es salaam kwa nia ya uchochezi alisambaza kwa umma nyaraka zilizosema “Kikwete kuuangamiza kabisa Ukristo. Kinyume cha sheria za nchi.

Katika shitaka la pili, Mtikila anadaiwa kuwa aprili 16 mwaka 2010 eneo la mikocheni Jijini Dar es salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka huo wa uchochezi.

Mchungaji Mtikila aliita mashahidi wawili akiwemo yeye mwenyewe, ambapo alidai mashitaka aliyoshitakiwa nayo sio sahii na kwamba , waraka aliousambaza na kumsababishia ashitakiwe , siyo wa uchochezi kwani umejaa maneno ya kumsifu Mungu.

Naye shahidi wa pili katika ushahidi wake, ambaye ni mpiga picha wa gazeti la mwananchi Mpoki Bukuku alisema kuwa ni kweli kampuni yao ilichapisha baadhi ya maneno yaliyokuwa kwenye waraka huo na hawakuwahi kulalamikiwa na polisi wala Mtikila mwenyewe.

Mara baada ya kushinda kesi hiyo lilizuka ‘timbwili’ lingine mahakamani hapo baada ya mtu mmoja kujitokeza akiwa na RB (Report Book) akimtuhumu Mchungaji Mtikila kuwa alimtishia kumuua na amemuibia kiwanja.

Baada ya kutaka kukamatwa na polisi mmoja aliyekuwa na cheo cha Koplo, Mchungaji alikataa kwa madai kuwa yeye ni kiongozi wa kitaifa hivyo hawezi kukamatwa na polisi mwenye cheo cha Koplo, labda polisi mwenye cheo cha SSP (Senior Superintendent of Police).

Kwa kauli hiyo polisi pia hawakumtia nguvuni.

SOURCE: RFA

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents