Habari

Elimu kwa mlipa kodi kuanza kutolewa mashuleni

Serikali imeona umuhimu wa kuingiza elimu ya mlipa kodi kwenye mitaala ya elimu nchini ili kwajengea Watanzania tabia, mwenendo na mazoea ya kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lupembe, Joram Ismael Hongoli juu ya kwa nini Serikali isiingize kwenye mitaala ya elimu somo la umuhimu wa kulipa kodi ili lifundishwe kuanzia shule ya msingi ili wananchi wapate uelewa wa kodi na waweze kulipa kodi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea.

“Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya mlipa kodi katika kumjengea mwananchi tabia ya kulipa kodi. Katika somo la Uraia na Maadili kuanzia darasa la III na kuendelea, mtaala umelenga kumjengea na kumuandaa mwanafunzi kuwa mwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku,” alisema Nasha.

Vile vile, mtaala umelenga kumjengea mwanafunzi kuiheshimu na kuithamini jamii yake kwa kuwa mwadilifu na mzalendo ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya kitaifa ikiwemo kulipa kodi.

Aidha amesema, kutokana na umuhimu wa kuwajengea vijana utamaduni wa kulipa kodi, elimu ya mlipa kodi ni jambo muhimu, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikisha Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) itaendelea kuboresha elimu hiyo ili isisitizwe na kuwekewa mkazo katika mitaala ya elimu kuanzia elimu ya Msingi.

Wakati huo huo, Nasha amesema Serikali ilifuta ada na michango ya lazima katika shule za umma ngazi ya elimu ya msingi (elimu ya awali hadi kidato cha Nne) na mpango huo hakuhusisha kidato cha tano na sita pamoja na shule binafsi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents