Burudani

Exclusive: Q Chief ajiondoa kwenye kampuni ya QS J Mhonda, Mhonda aelezea kilichotokea

Staa wa muziki nchini, Abubakar Katwila aka Q Chief amevunja mkataba wake na label ya muziki ‘QS J Mhonda’ kwa madai kuna vitu ambavyo haviendi sawa.

Q Chief

Chief ameiambia Bongo5 kuwa ameamua kujitoa rasmi katika label hiyo ili asimame mwenyewe.

“Mimi bhana naomba uwaambie mashabiki wangu pamoja na watanzania, sipo tena na QS J Mhonda,” amesema Q Chief. “Nimeamua kujitoa kwa sababu kuna vitu haviendi sana, sasa siwezi kuendelea kukaa bora nijitoe.”

Kutokana na hatua hiyo Bongo5 ilimtafuta Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mhonda aliyeeleza kwa upande wake kilichotokea.
“Kilichomuumiza Q Chief ni kuona mimi nawasaidia wasanii wengine,” amesema.

“Mimi kuwasaidia wasanii au watu mbalimbali ni sehemu ya maisha yangu sasa yeye amekuwa akisema hadharani mbele ya wasanii wangu wadogo kwamba hawapendi kuwaona wasanii wachanga anatamani hata kuwapiga bastola ili asiwaone kabisa. Nimejitaidi sana kumweka sawa ili aendane na mimi au na kampuni yangu lakini haonekani kubadilika na anaonesha roho mbaya kwa wenzake tena ya wazi,” ameongeza.

“Hivi karibuni niliamua kumuongeza Mzee Yusuf katika kampuni yangu yaani kuwa miongoni mwa wasanii wangu na nikampeleka Afrika Kusini kwa ajili ya video yake mpya, Q Chief akasirika kuona kwanini nafanya hivyo wakati hata kwake namfanyia hivyo hivyo na kuzidi. Kwahiyo sasa mimi binafsi hiyo taarifa imenishtua kwa sababu tayari nimeshatumia zaidi ya shilingi milioni 60 mpaka sasa na bado anakaa kwenye nyumba yangu. Nikimpigia simu ananiambia ‘ongea na mwanasheria wangu.’ Sasa mimi binafsi siwezi kulizungumzia hili suala na ni hatua gani tutazichukua lakini naomba ongea na mwanasheria wa kampuni yetu nadhani atakuwa na kauli.”

Bongo5 haikushia hapo, ilimtafuta mwanasheria wa kampuni hiyo, Joseph Mhina aliyedai kuwa mkataba ndio utamhukumu msanii huyo kwani kila kipengele kinaeleza hatua za kuchukuliwa endapo mteja atakiuka utaratibu.

Akiwa chini ya kampuni hiyo, Q Chief amefanya video mbili kubwa nchini Afrika Kusini zilizoongozwa na Adam Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents