Habari

Hiki ndio kitambulisho cha Rais wa Urusi Putin, kilichopatikana Ujerumani akiwa jasusi wa KGB (+Picha)

Kitambulisho cha Vladimir Putin alichopewa kama jasusi Ujerumani alipokuwa anafanya kazi kama jasusi wa Urusi kimepatikana katika makavazi mjini Dresden. Rais huyo wa Urusi amekuwa mara kwa mara akisema anajivunia kazi aliyoifanya akiwa kama jasusi wa idara ya ujasusi ya Urusi wakati huo ikifahamika kama KGB jijini Dresden miaka ya 1980. KGB kwa kirefu ni Komitet Gosudarstvennoy Bezopasnosti (Kamati/Idara ya Usalama wa Taifa)

Putin, wakati huo, alipewa kitambulisho na idara ya ujasusi ya Ujerumani Mashariki ambayo wakati huo ilikuwa chini ya Muungano wa Usovieti (USSR).  Idara ya ujasusi ya Ujerumani Mashariki ilifahamika kama Stasi, lakini kwa kirefu ni Ministerium für Staatsicherheit kwa maana ya maajenti wa Wizara ya Usalama wa Taifa.

Kwa mujibu wa BBC, Kitambulisho cha Stasi alichokitumia Putin kimegunduliwa wakati wa uchunguzi kuhusu ushirikiano wa karibu uliokuwepo kati ya KGB na Stasi. Putin ambaye wakati huo aikuwa na cheo cha meja katika KGB alipewa kitambulisho hicho kwama 1985 na kilimuwezesha kuingia kwenye afisi za Stasi, lakini si lazima iwe kwamba alifanya ujasusi kwa niaba yao.

Mihuri hii ni ishara ya miaka ya Bw Putin alivyoshirikiana na Stasi mjini Dresden kwa miaka kadha

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, maafisa wa Wakala wa Nyaraka za Stasi (BStU) walisema Bw Putin “alipokeza kitambulisho hicho ili kumuwezesha kufanya kazi zake za KGB kwa ushirikiano na Stasi.” Majasusi wa Stasi walifahamika sana kwa njia zao kali za ujasusi na jinsi walivyowapeleleza raia wa kawaida. Wakati mwingine waliwalazimisha watu wa kawaida kutoa habari kuhusu raia wenzao, hata wa karibu. “Utafiti wa sasa haujatoa ishara zozote kwamba Vladimir Putin alifanyia kazi Stasi,” taarifa ya BStU imesema.

Bw Putin alitia saini kama “Wladimir Putin”, jinsi linavyoandikwa jina lake kwa Kijerumani Bw Putin, alizaliwa Leningrad (mji ambao kwa sasa huitwa St Petersburg) na kwa sasa ana miaka 66. Alitumwa Ujerumani Mashariki kama jasusi mwaka 1985 akiwa na miaka 33. Mabinti zake wawili walizaliwa akiwa Ujerumani.

Putin alihudumu kama jasusi wa KGB mjini Dresden hadi Desemba 1989 pale utawala wa Kikomunisti wa Ujerumani Mashariki ulipoporomoka kutokana na maandamano ya kutetea demokrasia.

Kitambulisho chake cha Stasi kiliidhinishwa upya kila miezi mitatu, kama inavyoonyeshwa kwenye mihuri kwenye kitambulisho hicho. Haijafahamika ni kwa nini alikiacha kitambulisho hicho kwenye nyaraka za Stasi mjini Dresden.

Alikuwepo waandamanaji walipozingira na kutwaa udhibiti wa makao makuu ya Stasi mjini Dresden. Maafisa wa usalama wa kikomunisti waliokuwa wanalinda makao makuu hayo walikuwa karibu sana kuwafyatulia waandamanaji hao risasi siku hiyo 5 Desemba 1989.  Wakazi wa Berlin Mashariki iliyokuwa chini ya Ujerumani Mashariki walikuwa tayari wameuvunja na kuanza kuubomoa ukuta wa Berlin Novemba.

Bw Putin alikuwa anazungumza Kijerumani kwa ufasaha wakati huo na baadaye alisema aliitwa binafsi kujaribu kuwatuliza watu waliokusanyika na kuzingira afisi za KGB mjini humo. Aliwaonya kwamba ilikuwa ni ardhi ya Muungano wa Usovieti.

Wakati akifanya kazi na KGB mjini Dresden, Putin alipandishwa cheo hadi kuwa luteni kanali.

Vladimir Putin akiwa Dresden mwaka 2006

Mwaka 1989, alitunukiwa nishani ya shaba na Ujerumani Mashariki ikiwa bado chini ya utawala wa kikomunisti kwa “huduma yake na uaminifu wake katika kulitumikia Jeshi la Taifa la Wananchi”, inasema tovuti ya ikulu ya Urusi, Kremlin.

Ujerumani Mashariki kirasmi ilifahamika kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (GDR).

Baada ya kurejea Urusi, Bw Putin alipanda cheo na kuwa mkuu wa Idara ya Usalama wa Dola (FSB, kwa Kiingereza Federal Security Service) ambayo ndiyo iliyochukua nafasi ya KGB.

Alifanyia kazi meya wa St Petersburg kati ya 1990 na 1996, na baadaye akapanda cheo kisiasa hadi alipoteuliwa rais wa Urusi mwaka 2000.

Juni 2017, Putin alifichua kwamba kazi yake akiwa KGB ilijumuisha “kukusanya habari za kijasusi kwa njia haramu.”

Vladimir Putin akiwa na sare ya KGB.

Akizungumza na runinga ya taifa ya Urusi, alisema majasusi wa KGB walikuwa watu wenye “sifa za kipekee, kujitolea kwa hali ya juu na watu tabia za kipekee.”

Mkataba wa siri kati ya KGB na Stasi ambao BBC ilibahatika kuuona unaonyesha wakati mmoja KGB ilikuwa na maajenti 30 waliofanya kazi na Stasi Ujerumani Mashariki.

Putin akiwa katika mgahawa mmoja Dresden mwaka 2006

Msemaji wa ikulu ya Urusi Dmitry Peskov amepuuzilia mbali uzito wa taarifa za kupatikana kwa kitambulisho hicho cha Putin alichopewa na Stasi. “KGB na Stasi walikuwa mashirika mawili ya ujasusi yaliyokuwa na ushirikiano hivyo hauwezi kufutilia mbali uwezekano kwamba walibadilishana vitambulisho kama hivyo,” alisema.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents