Habari

Mahakama ya pili ya watoto nchini yazinduliwa

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma amezindua rasmi Mahakama ya watoto katika jiji la Mbeya na kufanya idadi ya Mahakama hizo nchini kufikia mbili. Mahakama ya kwanza ya watoto ikiwa Kisutu jijini Dar es salaam.

Mahakama hii ya Watoto iliyoanza kufanya kazi rasmi Aprili 18 mwaka huu jijini Mbeya pamoja na ile ya Kisutu zina kazi kubwa ya kuamua kesi za watoto wanaojikuta wana ukinzani na Sheria zinazohusu watoto nchini pamoja na kutafsiri sheria hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania alisema maendeleo endelevu ya Tanzania yatajengwa kwa misingi ya haki za watoto huku akinukuu andiko la shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto (UNICEF) lisemalo maendeleo ya taifa lolote yatakamilika baada ya watoto kuwa na afya njema, salama pamoja na kupata elimu.

Alisema uzinduzi wa jengo la Mahakama hiyo ya watoto unaashiria safari ndefu iliyonayo Tanzania ya kuhakikisha haki za watoto zinalindwa kwa kuwa pia bado kuna mikoa mingi ambayo inahitaji huduma hii muhimu.

Prof. Juma alisema kazi kubwa ya Mahakama ya Tanzania ni kutoa tafsiri pana ya sheria zinazohusu haki za watoto ili kupanua wigo wa ulinzi kwa watoto huku akiwataka Majaji na Mahakimu nchini kutafsiri sheria hizo ili zitekeleze wajibu wao kisheria.

Akitolea mfano wa Sheria ya Watoto namba 21 ya mwaka 2009, Kaimu Jaji Mkuu alisema sheria hii inashirikisha mihimili yote mitatu hivyo haki zote zinazotajwa na sheria hii ni lazima zipatikane inavyostahili. Prof. Juma pia amewataka Mahakimu wanaosikiliza kesi za watoto kuainisha mapungufu ya sheria hii na kuyawasilisha kwenye kamati ya Jaji Mkuu inayohusu masuala ya Sheria.

Aidha, Kaimu Jaji Mkuu amewataka Majaji na Mahakimu nchini wanaosikiliza kesi za watoto kujisomea zaidi masuala yanayohusu maendeleo ya haki za watoto kwa kuzisoma taarifa za utekelezaji za nchini pamoja na zile za nchi nyingine ili kupanua uelewa wa sheria hizo.

Kaimu Jaji Mkuu pia amewataka Majaji na Mahakimu wote kusimamia na kuhakikisha masuala yote yaliyotajwa na Sheria pamoja na mikataba ya kimataifa kuhusu watoto yanatekelezwa pindi wanapofanya ukaguzi kwenye magereza mbalimbali.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents