Burudani

Makala: Tujipange kutegua ‘Kitendawili’ cha Mrisho Mpoto na Kassim Mganga

Leo ni nimeamka na huyu mshairi mwenye tungo za aina yake katika tasnia ya muziki si mwingine namzungumzia, Mrisho Mpoto maarufu kama Mjomba Mjomba.

Msanii wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto.

Sitaki nikurudishe nyuma sana kule kwa ‘Nikipata Nauli’ na ‘Samahani Mwanangu’ kuliko jaa misemo na mashairi yenye kumfikirisha na kuacha maswali mengi kwa kila mtu.

Mwaka mmoja uliopita muimbaji huyo aliachia wimbo ‘Sizonje’ wenye ‘biti’ tamu kutoka kwa mtayarishaji mkongwe Alan Mapigo. Hebu tujikumbushe kidogo moja kati vesi za wimbo huo ulioacha maswali mengi kwa mashabiki.

[VESI 1 – MRISHO MPOTO]

Karibu sana Sizonje, hii ndo nyumba yetu
Tulipoficha mundu za kupondea wezi
Kwani, makaburi yaliofukuliwa lazima yazikwe upya?
Nyumba hii Sizonje ina vyumba vinne
Vitatu havifunguki, kimoja hakina mlango
Japokuwa kina watu ndani, na hawaongei Kiswahili.

Hakuna asiyeumiza kichwa kutaka kujua wazo la mwandishi na nia yake baada ya mashabiki wengi wa muziki kudai wimbo huo alimwimbia Rais John Pombe Magufuli.

Hata hivyo mshairi huyo hakuwahi kuthibitisha kama wimbo huo alimwimbia Rais Jonh Pombe Magufuli licha ya Rais huyo kutamka mara kadhaa kwamba wimbo huo ameimbiwa yeye.

“Sizonje namjua unataka nikwambie? Nitakwambia. Kuna sehemu uliimba vile vyumba vitatu visivyofunguka milango, sasa mimi nitakuonyesha funguo zake zilipo,” hayo ni maneno ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli akimwambia mkali wa mashairi ya kughani, Mrisho Mpoto.

Rais Magufuli hakuishia hapo: “Kati ya nyimbo ambazo nazipenda ni wimbo wako huu mpya wa Sizonje kwangu ni kama wimbo wangu wa taifa, naupenda sana, ni wimbo ninaosikiliza mara kwa mara.”

Kauli hiyo, ilikuja mara baada ya kushuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar alipokuwa akitokea Mwanza, ambapo alipokelewa na kikundi cha ngoma cha Mpoto na ndipo Magufuli alipopata nafasi ya kuzungumza kwa ufupi na msanii huyo.

Hiyo ni bahati ya kipekee kwa msanii kuzungumza na rais wa nchi na kupewa ujumbe huo.

Mpoto kwa sasa ameanza maandalizi ya ujio wake mpya na wimbo ‘Kitendawili’ akiwa amemshirikisha mkali nyimbo za mahaba, Kassim Mganga. Wimbo huo unatarajiwa kuachiwa Jumanne hii (August 1, 2017 ).

Msanii wa muziki, Kassim Mganga

Vitendawili ni tungo fupi ambazo huwa na swali fupi lisilo wazi na jibu kwa makusudi ya kupima ufahamu wa hadhira kuhusu mazingira yake. Anayetoa kitendawili huulizia swali lake kwa kutoa maelezo mafupi yanayorejelea umbo la kitu hicho, sauti, harufu au kukifananisha na kitu kingine. Anayejibu huhitajika kufikiria haraka na kutoa jawabu ambalo huwa la neno moja au maneno mawili hivi. Vitendawili huwa na mianzo maalum kulingana na jamii yake.

“Kitendawili ni wimbo ambao ni kitendawili kama jina lake, audio nitaiachia Agosti 1, mwaka huu, kiukweli sijawahi kuhisi kama ninaweza kufanya muziki wa tofauti na ukawa na ladha kama huu, mashabiki wangu mkae mkao wa kula msubiri kukitegua kitendawili siku hiyo,” amesema Mpoto na kuongeza: “Yawezekana ukanisikia kwenye singeli au ninachana au hata Taarab, ni staili gani nimekuja nayo hicho ndicho kitendawili chenyewe.”

Bila shaka wimbo ‘Kitendawili’ utakuwa ni wimbo wa mafumbo mengi kuanzia jina la wimbo hadi mashairi yake, inahitajika akili ya ziada kudadavua.

Huu ni wakati wa mashabiki kuanza kujipanga kutegua kitendawili hiko ili kupata madini iliyomo.

Mimi nakuachia Kitendawili: Nenda huko na nikirudi nimshike ngómbe wa mama mkia. Ukiwa na jibu komenti chini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents