Habari

Makamu wa Rais azitaka Taasisi kuacha kuajiri Wanunuzi na Wagavi wasiosajiliwa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mh. Samia Suluhu Hassan amezitaka Wizara na Taasisi kuacha mara moja kuajiri Wanunuzi na Wagavi wasiosajiliwa.

Makamu wa Rais aliyasema hayo leo, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 8 la Mwaka la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi lililofanyika kwenye kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Makamu wa Rais alisema “Nimefurahishwa sana na utamaduni huu wa kuwa na mkutano wa Wanataaluma ya Ununuzi na Ugavi kila mwaka. Ni utamaduni mzuri kwani unatoa fursa ya kujitathmini, kuelimishana na kuelezana mafanikio na changamoto mbalimbali katika kutekeleza shughuli za ununuzi na ugavi”.

Makamu wa Rais alitoa rai kuwa kongamano hili la siku mbili litumike kama fursa nyingine ya kukumbushana juu ya kuzingatia taratibu na sheria zinazosimamia masuala ya ununuzi na ugavi hapa nchini. Ni vyema mkaelezana ukweli, kuwekana sawa, kukemea bila uoga wala vitisho vitendo vyote vinavyotia doa taaluma pamoja na kuwawajibisha wale wote wanaochafua kada hii kwa kutekeleza majukumu yao kinyume na taratibu na sheria zilizopo. “Ni dhahiri kuwa watu hawa ni kansa kwa kada hii na hawafai kuwa miongoni mwenu; aidha wale wote watakaobainika kujihusisha na tabia hizo wachukuliwe hatua kali za kisheria.”

Pamoja na changamoto zilizopo bado kuna manunuzi ya ajabu yamekuwa yakifanyika kwa kutokuwa na bodi ya wazabuni na huu ni ukikukwaji mkubwa wa maadili alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais aliwaasa Wanunuzi na Wagavi kuwa Tunapozungumzia Tanzania ya viwanda isiwe sababu ya kuona ndio fursa ya kupata mlo ila tuhakikishe tunatumia pesa chache kwa kufanya mambo makubwa, kuwa wabunifu na waaminifu.

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha Sera ya Taifa ya ununuzi wa Umma mapema kwa kuwa ndiyo muongozo na msingi wa kufanya marekebisho ya Sheria.

Mwisho Makamu wa Rais alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha masuala mbalimbali katika kuikuza taaluma hii ya ununuzi na ugavi hapa nchini.

Wakati huo huo Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mpango amesema Wizara yake ndiyo yenye dhamana ya kusimamia ununuzi na ugavi hivyo itajitahidi kufanya kila linalowezekana kuimarisha taaluma ya ununuzi na ugavi sambamba na kuongeza nguvu kupambana na vitendo vinavyokinzana na maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi kama wizi, ubadhirifu, rushwa, upendeleo na kadhalika pia aliagiza uongozi wa PSPTB kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa wanataaluma wanaokiuka maadili na kujihusisha na vitendo vinavyoisababishia hasara Serikali.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents