Habari

Maseneta wa Marekani wanaamini Mwanamfalme Bin Salman alihusika mauaji ya Khashoggi

Maseneta nchini Marekani wanaamini pasi na shaka sasa kuwa mwanamfalme Mohammed bin Salman amehusika na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.

Msimamo huo wa maseneta unakuja baada ya kufanya kikao cha siri na mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, Bi Gina Haspel.

Seneta wa mwenye ushawishi mkubwa kutoka chama cha Republican Lindsey Graham amesema ana “imani ya hali ya juu” kuwa Mohammed bin Salman (MBS) alipanga njama ya kumuua Khashoggi.

Seneta huyo wa jimbo la Carolina Kusini amesema bin Salman ni “chizi” na “mtu hatari”.

Khashoggi aliuawa ndani ya ofisi za ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini Istanbul, Uturuki Oktoba 2. Mwanahabari huyo alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa sera za Saudia hususani mwanamfalme bin Salman.

Tayari Saudia imewashitaki watu 11 juu ya mauaji hayo, lakini wanakanusha vikali juu ya uhusika wa bin Salman.

Mkurugenzi wa CIA bi Haspel alikutana jana Jumanne na wajumbe wa Seneti wa Kamati ya Mambo ya Nje ambao hawakumung’unya maneno baada ya mkutano huo.

“Hapa hakuna bunduki inayofuka moshi – kuna msumeno unaofuka moshi,” amesema Seneta Graham akimaanisha mauaji ya Khashoggi yanayodaiwa kutekelezwa kwa kumny’onga kisha kumkata mwanahabari huyo vipande kwa kutumia msumeno.

Seneta Bob Menendez wa chama cha Democrat ameunga mkono msimamo wa Seneta Graham.

Mendez anayetoka jimbo la New Jersey amesema: “Marekani lazima itume salamu za wazi bila kubabaisha kuwa vitendo kama hivyo (mauaji) havikubaliki.”

Seneta mwengine kutoka chama cha Republican, akitumia jina maarufu la mwanafalme huyo la MBS amesema: “Sina hata swali moja kichwani mwangu juu ya kuwa MBS aliamuru mauaji hayo (ya Khashoggi).”

Seneta huyo meongeza kuwa : “Laiti MBS angesimamishwa mbele ya mahakama, angehukumiwa ndani ya dakika 30. Anahatia.”

CIA ‘yamlaumu bin Salman’ kwa mauaji ya Khashoggi

Seneta Corker ameonesha wasiwasi wake kuwa rais Donald Trump amepuuzia mauaji hayo kwa kushindwa kumlaani bin Salman.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents