Burudani

Mashabiki wamshambulia Bebe Cool kwa chupa jukwaani, mwenyewe adai Bobi Wine hakuumizwa anatafuta kiki

Msanii mkongwe wa muziki nchini Uganda, Bebe Cool wikiendi iliyopita amejikuta akikatisha show yake mjini Kampala baada ya kurushiwa chupa na mashabiki wake waliojawa na hasira ambao walihudhuria kwenye show ya tamasha lake la Swagz All Star.

Bebe Cool akishushwa jukwaani na Polisi mjini Kampala

Tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Kriketi vya  Lugogo, lilikatizwa ghafla na kelele za mashabiki waliosikika wakiimba ‘People Power’ huku wakirusha chupa na viti jukwaani, hali iliyopelekea askari polisi kupanda jukwaani kumshusha Bebe Cool.

Hata hivyo, muda mchache baada ya tukio hilo Bebe Cool kupitia ukurasa wake wa Facebook aliandika ujumbe mrefu akiwataka watu wa Uganda kuacha kuchanganya masuala ya kisiasa na muziki huku akihimiza uhuru wa mtu binafsi na demokrasia.

Vyombo vya habari nchini Uganda vimeeleza kuwa chanzo cha vurugu hizo, ni ukimya wa Bebe Cool wakati Bobi Wine alipokamatwa na jeshi la polisi huku wasanii wenzake karibia nchi nzima wakitumia hashtag ya #FreeBobiWine kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii wakishinikiza aachiwe huru.

Mapema jana Bebe Cool wakati akihojiwa na kituo cha runinga cha NTV Uganda, amesema kuwa msanii mwenzie Bobi Wine anajifanyisha tu kuwa na majeraha makubwa ili apate msaada wa huruma kutoka kwa wananchi wa Uganda na mataifa mengine duniani lakini hakupigwa alipokamatwa.

Bebe Cool amewataka pia watu wasiwe na mihemko ya kisiasa kwani kila mmoja ana haki ya kushabikia anachokitaka, hivyo kitendo cha yeye kukaa kimya kipindi Bobi Wine anakamatwa ulikuwa ni uamuzi wake binafsi.

Bebe ndiye msanii mkubwa nchini Uganda mwenye urafiki wa karibu na Rais wa taifa hilo, Yoweri Museveni na anatajwa kwa muda mrefu pia kuwa na tofauti za hapa na pale na Bobi Wine. Tazama video ya tukio hilo la kushambuliwa Bebe Cool
https://youtu.be/Fk-m5qoywCY

Related Articles

4 Comments

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents