Tupo Nawe

Matumaini ya Man United UEFA yafifia, Ole Gunnar asema anamatumaini ya kuifungaa Barcelona kwao

Manchester United inaweza kupata ushindi dhidi ya Barcelona wakiwa ugenini, kocha wa Mashetani Wekundu hao Ole Gunnar Solskjaer anaamini. Barca wameifunga United 1-0 katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dimbani Old Trafford, goli la Barcelona limepatikana katika dakika ya 12 baada ya mlinzi wa United Luke Shaw kujifunga.

Mchuano wa marudiano utafanyika dimbani Nou Camp Jumanne wiki ijayo.”Tunacheza na timu kubwa sana. Ni timu ngumu – tutaenda nyumbani kwao tukijua kuwa tutaweza kushinda kule,” Solskjaer amekiambia kituo cha runinga cha BT Sport.

“Tunaenda kule tukiwa na kitu kimoja tu kichwani: tunatakiwa kushinda.”

Katika hatua ya mtoano, United walionekana kana kwamba wameshayaaga mashindano baada ya kupoteza kwa goli 2-0 dhidi ya Paris St-Germain wakiwa nyumbani, lakini wakawaacha watu midomo wazi baada ya kwenda kupata ushindi wa 3-1 nchini Ufaransa, na kufanikiwa kuendelea kwa faida ya goli magoli la ugenini.

“Kiwango tulichokionesha dhidi ya PSG kinatupa matumaini kuwa tunaweza, lakini tunacheza na timu inayopigiwa chapuo zaidi,” amesema Solskjaer.

Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde pia amedai ni ngumu kusema United wameshang’oka.

“Tazama namna walivyofanya jijini Paris (dhidi ya PSG), inabidi utazame tu walichokifanya pale – haya matokeo ya 1-0 bado si ya mwisho,” amesema Valverde.

Atakayepita atakutana na Liverpool ama Porto katika hatua ya nusu fainali.

Klabu Bingwa 2018-19
Magoli ambayo Barcelona wamefungwa nyumbani2
Magoli ambayo Manchester United wamefunga ugenini9

Juventus waibana Ajax

Cristiano Ronaldo

Juventus wamefanikiwa kupata sare ya 1-1 wakiwa ugenini dhidi ya Ajax, jijini Amsterdam, Uholanzi.

Ronaldo amepachika goli hilo katika dakika 45′ kwa kichwa safi, na kufikisha magoli 125 akiendelea kuchanja mbuga kama mchezaji mwenye magoli mengi zaidi kwenye historia ya michuano hiyo.

Ronaldo amefunga magoli hayo akiwa na timu tatu, awali Manchester United halafu Real Madrid na sasa Juventus.

Mchezaji huyo nguli amenyanyua kombe hilo mara tano.

Ajax walisawazisha dakika moja tu baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia David Neres kwa shuti la yadi 15.

Timu zote mbili zilipata nafasi za wazi ambazo walishindwa kuzitumia. Jurgen Ekkelenkamp wa Ajax alipata nafasi ya wazi ambayo iliokolewa kabla ya nafasi ya Douglas Costa wa Juventus kugongesha mwamba.

Sasa timu hizo zitaenda kumalizana mjini Turin, Italia juma lijalo.

Atakeibuka mshindi atakutana na mmoja wapo kati ya Man City na Tottenham katika hatua ya nusu fainali.

Wafungaji Bora wa Klabu Bingwa Ulaya
JinaMagoliTimu
1. Cristiano Ronaldo125Manchester United, Real Madrid, Juventus
2. Lionel Messi108Barcelona
3. Raul71Real Madrid, Schalke
4. Karim Benzema60Lyon, Real Madrid
5. Ruud Van Nistelrooy56PSV Eindhoven, Manchester United, Real Madrid
6. Robert Lewandowski53Borussia Dortmund, Bayern Munich
7. Thierry Henry50Monaco, Arsenal, Barcelona
8. Andriy Shevchenko48AC Milan, Chelsea, Dynamo Kiev
8. Zlatan Ibrahimovic48Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, AC Milan, Paris St-Germain
10. Filippo Inzaghi46Juventus, AC Milan

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW