Habari

Meya auawa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya

Meya wa jiji la Ozamiz nchini Ufilipino, Reynaldo Parojinog ambaye anatuhumiwa na Rais wa nchi hiyo, Rodrigo Duterte kuwa anajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ameuawa katika msako wa Jeshi la polisi.

Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte

Reynaldo Parojinog ameuawa kwa kupigwa risasi pamoja na mkewe na watu wengine 10, pale nyumba yake ilipovamiwa na askari.

Polisi wanasema, walikuwa wakisaka katika nyumba hiyo, kukabidhi waranti ya kumkamata Meya huyo ndipo utumiaji nguvu ukazuka.

Watu karibia elfu 9 wameshauawa katika misako ya polisi, au wameuliwa na magenge ya wanamgambo, tangu Rais Duterte kuingia madarakani mwaka jana, kufuatia kampeni ya uchaguzi, ambapo aliahidi kuua maelfu ya watu ili kufyeka biashara ya mihadarati nchini Ufilipino.

Katika msako huo Polisi walipata bunduki, pesa na madawa ya kulevya kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa Ozamiz, Kamanda Jaysen De Guzman.

Bwana Porojinog ni Meya wa tatu kuuawa katika harakati kali za Serikali kukabiliana na madawa ya kulevya, ambapo Rais Duterte amewataja maafisa, polisi na majaji kuhusika kwenye biashara hiyo.

Hatua hiyo imempa umaarufu  Rais Duterte duniani ingawaje imekoselewa na makundi ya kupigania haki za binadamu ulimwenguni kwa kukemea kitendo hicho.

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents