Habari

Mwanafunzi anaswa na polisi baada ya kumkaba mama yake mzazi na kumpora

Jeshi la Polisi jijini Dodoma linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari ya Itega, Mohamed Ramadhani (18) kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu ikiwa ni pamoja na kumkaba mama yake mzazi.
Mwanafunzi huyo anatuhumiwa kujiunga na kikundi cha uhalifu cha Kamchape ambacho kinajihusisha na ukabaji na uvunjaji katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa jiji la Dodoma, Gilles Muroto alisema kuwa kijana huyo amekuwa akijishughulisha na uhalifu ambapo kwa siku za hivi karibuni aliwahi kukiri kumkaba mama yake mzazi lakini mama huyo hakujua kuwa aliyemkaba ni mwanaye.
“Huyu kijana alijua kuwa aliyemkaba na kumpora ni mama yake mzazi, hivyo alivyogundua  aliyempora ni mama yake alichofanya ni kumwachia mkoba aliompora na kutokomea kusikojulikana bila yule mama kufahamu, kuwa aliyemkaba ni mwanaye wa kumzaa”, alisema Muroto
Aidha, Kamanda Muroto alisema baada ya tukio hilo kijana huyo aliachiwa lakini alikamatwa tena, alipobainika kuwa amehusika katika kuvunja nyumba ya mtu na kuwafunga kamba wenye nyumba ili wawaibie.
Kwa upande wake, mtuhumiwa huyo amedai chanzo cha yeye kujihusisha na matukio hayo ya uhalifu ni kutokana na hali ngumu ya maisha ndio imemfanya kutenda hayo.
“Nina ishi na mama peke yake hivyo sina mtu wa kunihudumia viatu vya shule, madaftari, vitabu, sare za shule na mahitaji mengine ndiyo maana nakaba watu ili nipate mahitaji hayo” alisema Mohamed ambaye hadi sasa bado anasoma katika shule ya sekondari Itega kidato cha tatu.
Wengine wanaounda kundi hilo la Kamchape lililopo Kizota ni Abdul Mchangala (18), Mashaka Idd (17), Salum Mohamed (24) na Hamis Kikweli (40).
Kamanda Muroto ametoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika mkoa wa Dodoma pamoja na wale wanaonunua vitu kutoka kwa wahalifu kuwa adhabu kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents