Habari

Petroli yashuka, dizeli, mafuta ya taa yapanda

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (EWURA) imetangaza kushuka kwa bei ya petroli huku dizeli na mafuta ya taa vikipanda kwa wastani wa shilingi saba hadi 12 kwa lita moja.

Bei hiyo ni tofauti ikilinganishwa zilizotangazwa Machi Mosi mwaka huu. Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi Dar es Salaam jana ilieleza kuwa bei hiyo itaanza kutumika rasmi hii leo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa bei ya rejareja ya petroli imepungua kwa shilingi tatu kwa lita moja sawa na asilimia 0.13, huku bei ya jumla ikishuka kwa Sh 5.65 kwa lita au asilimia 0.29.

Wakati petroli ikishuka, bei ya dizeli imepanda kwa Shilingi 12 kwa lita moja sawa na asilimia 0.63, bei ya jumla imeongezeka kwa Shilingi 9.11 kwa lita sawa na asilimia 0.50.

“Bei ya rejareja ya mafuta ya taa imepanda kwa Sh saba kwa lita sawa na asilimia 0.36 ambako bei ya jumla imepanda kwa Sh 3.68 kwa lita sawa na asilimia 0.21.”

“Kwa kiasi kikubwa, mabadiliko haya ya bei yametokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, mfumuko wa bei na gharama za usafirishaji (BPS Premiums) ikilinganishwa na mwezi uliopita,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Imesema Machi mwaka huu hakuna mzigo wa mafuta uliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Tanga. “Ongezeko hilo la bei za mafuta linatokana na ongezeko la faida ya wauza mafuta wa jumla na rejareja kutokana marekebisho yaliyofanywa kukidhi matakwa ya mfumko wa bei kwa mujibu wa kanuni ya ukokotoaji wa bei za mafuta katika mwaka 2016,” iliongeza taarifa hiyo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents