Picha: Zanzibar yakumbwa na mafuriko, misaada ya kibinadamu inahitajika
Mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kali iliyonyesha kuanzia jana Jumapili na kuendelea hadi leo, yamesababisha maafa makubwa vikiwemo vifo na watu wengi kupotea makazi.
Eneo la uwanja wa ndege visiwani humo likiwa limejaa maji
Taarifa zinadai kuwa hadi sasa watu wawili wanadaiwa kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo. Nyumba nyingi zimejaa maji yaliyosababisha hasara kubwa.
Wananchi wakijaribu kuendelea na shughuli za kawaida licha ya maji kujaa hadi kufikia maeneo ya kiunoni
Akiongea na Bongo5, mmoja wa watu wanaounda timu inayoshughulikia masuala ya misaada ya kibinamu kwa waathirika, Arafat, amesema watu wengi wanahitaji misaada mbalimbali.
Barabara na miundombinu mingine imeathirika
“Jana ndio hali ilikuwa mbaya zaidi nyumba nyingi zilijaa maji zingine zilibomoka kutokana na nguvu ya mvua na wingi wa maji,” amesema.
Ameyataja maeneo yaliyoathirika zaidi na mafuriko ni pamoja na Kariakoo, Jang’ombe, Msendawe na Raha Leo. Arafat amedai kuwa pamoja na baadhi ya waathirika wa mafuriko kupewa hifadhi na ndugu zao, wapo waliokosa kabisa mahali pa kuishi hivyo wanafanya jitihada za kuwatafutia eneo moja la kuwahifadhi kwa muda.
Maji kwenye uwanja wa ndege yakiwa yamepungua baada ya kujaa
Ametaja mavazi, misaada ya vyakula, vifaa vya afya na madawa ndio vitu vinavyohitajika zaidi kwa sasa.
Kama umeguswa na unapenda kusaidia chochote, wasiliana na namba hizi. -0767278381 (Arafat) na Aysha- 0777888888.
Chini ni picha zingine za mafuriko hayo.