Habari

Polisi yaongeza nguvu kuchunguza mlipuko bomu katika mkutano wa CHADEMA Arusha

KUFUATIA mlipuko wa bomu uliotokea juzi katika mkutano wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Arusha na kuua watu wawili na majeruhi zaidi ya 60, jeshi la Polisi nchini limeunda timu ya maofisa kutoka makao makuu Dar es Salaam ili kuongeza nguvu ya uchunguzi wa mlipuko wa bomu hilo.

196459_10201527423173761_1596527095_n
Majeruhi wakiwa kwenye eneo ulipotokea mlipuko huo

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP. Said Mwema amesema imeteua maofisa hao ili kwenda kuongeza nguvu za uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo la mlipuko wa bomu uliotokea Soweto, Kata ya Kaloleni Arusha.

Alisema timu hiyo ya uchunguzi inayoenda kusaidiana na wengine kutoka Mkoani Arusha, inajumuisha makamishna wawili kutoka Operesheni na Idara ya Upelelezi Makao Makuu, itaongozwa na Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Kamishna Issaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi Makosa ya Jinai.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza jana alisema uchunguzi wa tukio hilo unahusisha vikosi vyote vya usalama nchi likiwemo Jeshi la Wananchi (JWTZ) kubaini wahalifu hao ambao wanatishia usalama wa nchi na raia wake.(Source: thehabari.com)

z6

Gazeti la leo la Mwananchi limeandika kuwa taarifa iliyotolewa na Ikulu jana imeeleza kuwa Rais Kikwete ambaye yuko nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa nchi zilivyoendelea kiviwanda(G8), alisema haamini kama Watanzania ama wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kudiriki kufanya matukio ambayo yanahatarisha usalama wa watu.

“Mimi siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii. Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema nchi yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni mwa raia ama makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko makubwa.”

999875_535514443179221_429038972_n

Kwa upande wake Mwenyekiti (CHADEMA) Taifa na kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe alisema shambulio hilo la bomu ni la kisiasa na lililenga kumuua yeye na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema.
“Haya ni mauaji ya kisiasa ya kupanga, tumeokota maganda ya risasi za bastola na SMG na tumepiga picha na kuwapa polisi katika eneo la tukio, gari letu lilipigwa mlango na vioo kwa risasi na kesho wabunge wote wa Chadema watakuwa hapa Arusha na wataondoka baada ya mazishi,” gazeti la Mwananchi limemnukuu Mbowe.

Hii ni mara ya pili kwa Jiji la Arusha kushambuliwa kwa bomu baada ya lile lililorushwa kwenye Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi kwenye Parokia ya Olasiti wakati wa sherehe ya uzinduzi wake Mei 5, mwaka huu na kuua watu watatu na kujeruhi 64.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents