Rich Mavoko asainishwa na kampuni ya usimamizi ya Kenya inayomsimia pia Avril
Rich Mavoko amesaini mkataba na kampuni ya usimamizi ya Kenya iitwayo Kaka Empire iliyoanzishwa na rapper Rabbit.
Kampuni hiyo pia inawasimamia wasanii wa Kenya akiwemo Avril, Raj, FemiOne na Owago.
Mavoko ameiambia Bongo5 kuwa kampuni hiyo itakuwa ikisimamia kazi zake zote kwa upande wa Kenya peke yake.
Amedai kuwa uamuzi wa kuamua kuwa chini ya kampuni hiyo umekuja baada ya kubaini kuwa ana mashabiki wengi nchini Kenya na kuna watu wamekuwa wakifaidika kwa kuuza kazi zake bila yeye kufahamu.
“Nimekuta mdundo.com kuna mtu anachukua hela zangu tangu miaka mitatu nyuma, tangu nyimbo ya Silali. Sio hela ndogo, ni dola kadhaa. Yule jamaa alienda kujitambulisha kwamba yeye ni meneja wangu,” amesema Mavoko.
“Kwahiyo jamaa wakaniambia kwamba hakuna mtu anayeweza kufuatilia vitu vyako vya Kenya kwahiyo inabidi upate wakala au mtu anayeweza akasimamia kazi zangu za Kenya naye atakuwa anachukua asilimia lakini haki zako zote unazipata,” ameongeza.
Rich akiwa na Rabbit
Hivi karibuni Rabbit aka Kaka Sungura alimshirikisha Mavoko kwenye wimbo wake ‘Njoo’.