Habari

Tanzania na Ethiopia wakubaliana kushikamana kiuchumi

Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia, Mhe Hailemariam Dessalegn amemhakikishia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania utakaosaidia kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi.

Waziri Dessalegn ametoa kauli hiyo Ijumaa hii, Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa Tanzania na Ethiopia kupitia vyombo vya habari muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili, anayoifanya kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Dessalegn alisema “Shirika letu la ndege la Ethiopia ni shirika linaloendeshwa kwa faida Barani Afrika, lina ndege 96 na linatarajia kununua ndege nyingine 42, ndege zake zinatua katika viwanja 92 duniani kote na viwanja 42 ndani ya Ethiopia, hivyo nitawaleta viongozi wa shirika hili ili waje washirikiane na ATCL kuweka mkakati wa namna ya kuiendeleza ATCL na kuiwezesha kufanya kazi kwa faida.”

Waziri huyo alisema shirika la Ndege la Ethiopia kwa kushirikiana na ATCL litaufanya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuwa kituo chake cha mizigo (Cargo Hub) na hivyo kuwezesha mizigo ya ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo jirani kutumia uwanja huo kusafirisha mizigo yake duniani kote.

Kabla ya mazungumzo Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Hailemariam Dessalegn walifanya mazungumzo rasmi, walisema wamekubaliana kuwa Tanzania na Ethiopia zibadilishane uzoefu juu ya uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia maji ambapo Mhe. Hailemariam Dessalegn aliahidi kuwatuma wataalamu wa nchi yake kuja nchini Tanzania kutoa uzoefu wa namna Ethiopia ilivyoweza kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kwa kutumia maji.

Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia, Mhe Hailemariam Dessalegn yuko nchi Tanzani katika ziara yake ya kiserikali kwa mwaliko aliopewa na mwenyeji wake Rais Magufuli.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents