Habari

TBA wamuondoa kigogo ujenzi wa hospitali

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umechukua hatua za haraka, kwa kumuondoa kwenye nafasi yake Meneja wa Mkoa wa Simiyu, Michael Semfuko na kumrejesha Makao Makuu Dar es Salaam kupisha uchunguzi.

Uamuzi wa kumng’oa meneja huyo wa mkoa, uliwekwa wazi Dar es Salaam jana na Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu, kuzungumzia mradi huo pamoja na kutembelea miradi inayosimamiwa na TBA, ikiwa ni agizo alilopewa Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka na Rais.

“Kisheria miradi yote ya ujenzi kwenye mikoa yote huwa inasajiliwa TBA, lakini cha kushangaza mradi huu haukuwa umesajiliwa na sielewi, lakini sitaki kusemea tutakapofika huko tutajua ni kwanini imekuwa hivyo. Inawezekana meneja alipewa mradi siku hiyo au alikuwa anaupitia ili aulete kwetu, yote hayo tutayajua baada ya maelezo yake,” alisema Mwakalinga.

Akizungumzia zaidi mradi huo wa Simiyu, alisema wameunda kamati kwa ajili ya kupitia upya mchoro uliokuwepo na kuandaa utaratibu ili kuanza mchakato wa ujenzi kwa kuwa tayari Rais alishazungumza hivyo unapaswa kutekelezwa.

Wiki iliyopita Rais Magufuli akiwa ziarani Simiyu, aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, lakini hakukubaliana na gharama ya shilingi bilioni 46 iliyotajwa ili kukamilisha mradi huo badala yake alitaka ijengwe kwa shilingi bilioni 10.

BY: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents