Habari

Trafiki waanza kupiga tochi usiku, madereva 20 wanaswa

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini limeanza kuwakamata madereva wanaoendesha magari kwa kasi wakati wa usiku na tayari madereva 20 wamenaswa kwa kutumia tochi.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim aliliambia Mwananchi jana kuwa, wameanza kukagua magari nyakati za usiku baada ya kubaini madereva aliowataja kuwa ni wakorofi kuhamishia ‘vurugu’ za mwendo kasi usiku.

Alisema baadhi ya madereva huvunja sheria muda huo wakidhani Jeshi la Polisi halipo kazini.

“Tunakagua (magari) usiku na mchana na hao madereva wanaolalamika (kukamatwa usiku) tutawanyakua wakati wowote, mwendokasi wa mchana sasa hivi wameuhamishia usiku, kwa hiyo tutawakamata na kuwafungia leseni zao, haiwezekani ajali ziendelee kupoteza maisha ya watu kwa uzembe wa mtu mmoja,” alisema Muslim.

Alisema Novemba 30 walianza kuwakamata madereva wanaoendesha kwa kasi na kwamba, zaidi ya madereva 20 wameshanaswa kupitia tochi kati ya saa 4:00 usiku na kuendelea wilayani Same mkoani Kilimanjaro na Arusha.

Baadhi ya madereva waliozungumza na Mwananchi wamekilaumu Kikosi cha Usalama Barabarani kuwa kinafanya kazi zake kwa kuvizia.

Mmoja wa madereva hao, Shija Bujiku alisema alipigwa tochi saa nne usiku akitokea Arusha kwenda Dar es Salaam kuandikiwa faini ya Sh30,000 kutokana na kosa la mwendo kasi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents