Habari

Video: Mambosasa ateta na wakazi wa Mbagala, akutana na jibu la askari Faru John

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa Jumapili hii alikutana na wakazi wa Mbagala Zakhem Jijini Dar es salaam na kuzungumza nao kuhusu kero mbalimbali za kiusalama na wakazi wa eneo hilo pamoja na kuzitolea ufumbuzi.

Kamanda Mambosasa akisalimiana na wakazi wa Mbagala

Wananchi wao walipata fursa ya kumueleza kamanda huyo kero zao ambapo moja ya kero ambayo iliibuliwa ni tuhuma juu ya polisi aliyepachikwa jina la Faru John kuwanyanyasa wananchi kwa kuwafunga pingu ovyo pamoja na kuwamba rushwa na tsh 20000

Amesema huo ni mmomonyoko wa maadili kwa askari ambao kazi yao ni kulinda raia na mali zao, hivyo atawachukulia hatua wote watakaobainika kuomba na kupokea rushwa.

“Ninawaomba askari kuwalinda wafanyabiashara wenye mitaji midogo kama vile wakaanga chipsi. Kuwadai Sh20,000 eti kwa sababu wamechelewa kufunga biashara hilo sikubaliani nalo hata kidogo, lazima niwachukulie hatua,” amesema Kamanda Mambosasa.

Pia, amekemea askari wanaodai rushwa kwenye vituo vya polisi ambavyo amesema vipo kwa ajili ya kutoa huduma.

Amewaagiza wakuu wa vituo kuhakikisha watu hawakai muda mrefu vituoni kwa kuwa kufanya hivyo ni kutengeneza mazingira ya kupokea rushwa.

Mkazi wa Mbagala, Thabiti Mohamed alisema kuna askari anayejulikana kwa jina la Faru John amekuwa akiwakamata wafanyabiashara, wakiwemo wauza chipsi ambao huchelewa kufunga maduka hadi saa tano usiku na huzunguka nao usiku kucha wakiwa wamewafunga pingu.

Mohamed alisema askari hao huomba kwanza Sh20,000 ili kuwaachia na wasipozitoa ndipo hufungwa pingu na kupakiwa kwenye gari.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibangulile, Mashaka Selemani amemuomba Kamanda Mambosasa kuwahamisha askari wa Kituo cha Polisi Maturubai akisema hawakamati wahalifu bali wapo kwa ajili ya kupokea rushwa.

“Askari hawa kazi yao wanapomkamata mtuhumiwa wanampeleka ofisi ya Serikali ya Mtaa Mikwambe, wanapofika kazi yao wanataka fedha kwa nguvu. Wasipopata wanawapiga na kuwabambikia kesi. Tumefuatilia wanakusanya hadi Sh1 milioni kwa siku, hivyo wameshazoeleka tunataka waondolewe Mbagala,” alisema Selemani.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents