Habari

Viongozi wa Chadema wahojiwa kwa saa 5, watoka kimya kimya

Ilichukua takribani saa tano kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho, kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kuanzia saa 7 mchana hadi sasa 12 jioni.

Viongozi hao wakiingia kituoni hapo jana mchana

Viongozi hao walifika kituoni hapo ili kuitikia mwito wa kuwataka kufika katika kituo hicho, uliotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Katika tukio lingine jana, Chadema ilitangaza kufungua kesi namba 31 ya mwaka huu ikiwa na madai mbalimbali dhidi ya Jeshi la Polisi.

Februari 20, kamanda huyo aliwataka viongozi saba wa chama hicho wakiongozwa na Mbowe kufika katika kituo hicho, baada ya kudaiwa kufanya maandamano bila kibali, ambayo yaliyosababisha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilin (22) kufa kwa kupigwa risasi akiwa katika daladala wakati wafuasi wa chama hicho wakiandamana.

Maandamano hayo yalifanyika Februari 16, mwaka huu, baada ya kumalizika kwa kampeni za uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Kinondoni, ambapo wafuasi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe, walikuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai barua za mawakala wa chama hicho za kusimamia uchaguzi .

Maandamano hayo yalianzia viwanja vya Buibui, Mwananyamala, ulikokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni wa Chadema na yalipofika eneo la Mkwajuni, yalitawanywa na Jeshi la Polisi.

Viongozi walioambatana na Mbowe ni Manaibu Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalim (Zanzibar), Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, Mwenyekiti Kanda ya Serengeti, John Heche na Mweka Hazina wa Bawacha, Esther Matiko.

Mdee, Mnyika na Heche walisharipoti kituoni hapo na kuhojiwa, ambapo walitakiwa kurejea tena jana. Viongozi hao waliwasili kituoni hapa majira ya saa 6:50 mchana baada ya kumaliza kufanya mkutano wao na waandishi wa habari, ambapo Mbowe alitangaza kuwa atakwenda katika kituo hicho kutii mwito.

Alidai kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji hatofika katika kituo hicho, kwa kuwa yupo nje ya nchi. Majira ya saa 12 jioni mmoja wa walinzi wa viongozi hao, aliyetoka katika kituo hicho, alidai kuwa tayari viongozi wengine wameshahojiwa, lakini Mbowe bado alikuwa ndani akiendelea na mahojiano.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents