Habari

Vyuo 15 vyatakiwa kuwasilisha matokeo ya mitihani

Serikali imetoa siku mbli kwa vyuo vikuu 15, kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo wanaoendelea na masomo ili kupangiwa mikopo kwa mwaka wa 2016/2017.

picdrslakwanza

Vyuo hivyo vilivyokuwa viwasilishe matokeo hayo siku 30 kabla ya kufunguliwa, vimepewa siku hizo kuanzia Jumanne hii, kabla serikali haijachukua hatua zozote. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi alisema hayo Jumanne hii, alipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa elimu ya juu.

Tarishi alisema baadhi ya vyuo vimeshindwa kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa wanafunzi wanaoendelea ili wapangiwe mikopo kwa mwaka unaoendelea, kwani utaratibu lazima vyuo kuwasilisha matokeo kuonesha wanafunzi wangapi wana sifa za kuendelea kupewa mikopo.

“Bodi ya mikopo ipo katika hatua ya mwisho za utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu lakini katika utekelezaji huo tumepata changamoto kwa baadhi ya vyuo na vyuo hivyo viko jumla yao 15 ambavyo havijaleta matokeo ya mitihani kwa wale wanafunzi wanao endelea kwahiyo bodi inashindwa kuendelea na malipo,”alisema Tarishi.

Tarishi alivitaja vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo hayo kuwa ni Vyuo vya Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma, Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UOB), Chuo Kikuu cha St. John Kituo cha St Mark Dar es Salaam (SJUTDSM), Chuo cha St. John Tanzania (SJUT) na Chuo Kikuu cha Tumaini Mbeya (TUMAMBEYA).

Vingine ni Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI), Chuo cha United African University of Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha Tiba ya Sayansi (STJCAHS), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Kituo cha Makambako na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).

Serikali ya awamu ya tano imesema imejipanga kikamilifu na imetenga fedha za kutosha na tayari imetoa shilingi bilioni 80.89 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, wanaonufaika na mikopo hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents