Habari

Waziri Majaliwa ahimiza maendeleo ya viwanda

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji katika mikoa yote nchini kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya viwanda mbalimbali katika maeneo yao.

Amesema mpango wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuinua uchumi wa Taifa kutoka wa chini kwenda wa kati, hivyo ni muhimu kuvifuatilia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo alipozungumza na watendaji na wananchi wa mkoa wa Morogoro alipofanya ziara katika kiwanda cha Moproco.

Alisema licha ya kukuza uchumi wa Taifa, viwanda vitasaidia katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana kwani vinauwezo wa kuajiri watu wengi.

“Viwanda hivi vinatupa uhakika wa ajira nchini kwa sababu vinauwezo wa kuajiri watu wengi na wa kada mbalimbali, hivyo ni muhimu tukafuatilia utendaji wake,” alisema Waziri Majaliwa.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa mbali na kutoa ajira nyingi, pia viwanda vitawezesha wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao na kukifanya kilimo kuwa na tija.

Alisema kwa muda mrefu sekta ya viwanda nchini ilikuwa haifanyi vizuri jambo ambalo lilisababisha kuongezeka kwa tatizo la ajira na mazao yalikosa soko.

Hata hivyo Waziri Mkuu alitoa wito kwa wafanyakazi walioajiriwa katika viwanda mbalimbali kuwa waaminifu ili kuviwezesha viwanda hivyo kuendelea na uzalishaji.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage pamoja na maofisa wengine wa Serikali.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents