Habari

Waziri Mkuu ahimiza wakazi wa Lindi kujipanga maandalizi ya Baraza la Maulid Kitaifa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watu wa mkoa wa Lindi watumie fursa zilizopo ili kufanikisha maandalizi ya sherehe za Maulid na Baraza la Maulid Kitaifa mwaka huu.

Waziri Mkuu, ametoa wito huo Jumapili hii, wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.

“Kwa niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mheshimiwa Mufti na Baraza la Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa wilayani kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika sherehe hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” alisema Majaliwa.

Aidha Waziri Mkuu, aliwataka wana-Ruangwa waharakishe kujenga nyumba za kulala wageni na sehemu za kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa. “Kila mmoja anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataarifu viongozi hao kwamba maandalizi yanaendelea na kwamba vifaa mbalimbali kama mchele, vitoweo, unga wa ngano, sukari, maji, juisi, mahema, mikeka na mazulia vimeishapatikana.

“Ninaomba Kamati ya Uhamasishaji ifanye kazi hii kwa kutambua kuwa jambo hili si la kwenu peke yenu, bali linaungwa mkono na Serikali, na hii ni kwa sababu Serikali yenu inafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa dini,” alisema.

Waziri Mkuu amesema sherehe hizo zitafanyika Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, saa 3 asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents