Habari

Waziri Mkuu awabana Maafisa kilimo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa kilimo na maafisa ushirika wa mkoa wa Tabora wasimamie kwa umakini ukuzaji wa zao la tumbaku kuanzia msimu ujao.

“Mkakati wetu wa kuinua zao hili unaanza msimu ujao, ninaondoka Tabora lakini nataka kila mmoja wenu atumie nafasi yake kuelezea suala hili kwa kina kwa wakulima wa zao la tumbaku ili tubadilishe mfumo na tuweze kuwakomboa,” alisema.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya za mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum.

“Tumieni vyombo vya habari kila mmoja apange ratiba kuelezea atafanya nini, toeni elimu kwa sababu vyombo hivi vinasikika hadi kwenye mikoa ya jirani,” alisisitiza.

“Afisa kilimo wa wilaya lazima ujue una wakulima wangapi, je wakulima wako kila mmoja analima ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana mahitaji ya pembejeo kiasi gani?” alieleza Waziri Majaliwa.

“Afisa ushirika wa wilaya nawe hakikisha unasajili idadi ya vyama vya msingi (AMCOS) vilivyoko kwenye eneo lako, lazima ujue AMCOS ziko ngapi na zina wanachama wangapi. Afisa kilimo na afisa ushirika muanze kazi hiyo mara moja,” alisisitiza.

“Ulizeni mahitaji yao ni yapi, kwa kila mwanachama na kila AMCOS, kisha muziwasilishe kwa Mkuu wa Mkoa ili naye azifikishw kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Pale wizarani, tunataka Mkurugenzi wa Pembejeo ajue mahitaji ya kila mkoa ili pembejeo ziweze kuwasilishwa kwa wakulima miezi miwili kabla msimu wa kilimo haujaanza, kama ambavyo tumeagiza,” alisema.

Akifafanua kuhusu uagizaji wa mbolea, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanzisha mfumo wa pamoja wa mbolea (bulk procurement) na akawataka wataalamu wa wizara ya kilimo wamalize mgogoro wa siku nyingi uliokuwepo baina yao na kiwanda cha mbolea cha Minjingu.

“Kumekuwa na maneno maneno kuhusu mbolea ya NPK, lakini wakati sisi tunaidharau, wenzetu wa nchi jirani wanaongoza kwa kuagiza mbolea nyingi kutoka Minjingu. Acheni kuagiza mbolea hiyo kutoka nje ya nchi, tukachukue pale Minjingu,” alisisitiza.

Alisema mwenye kiwanda ameahidi kwamba akipewa oda ya mbolea, yeye atazisafirisha hadi kiwandani. “Hakuna haja ya kuwaumiza wakulima na mbolea za bei mbaya wakati tunayo hapa nyumbani na tena ya bei nafuu. Wenye makampuni ya kununua tumbaku wanauza mfuko mmoja kwa dola 70 sawa na sh.150,000 hii ya Minjingu yenye ubora uleule inauzwa sh. 60,000 kwa mfuko mmoja, tena zikiwa zimefikishwa wilayani.”

“Ninawasihi viongozi wa ushirika na wa wilaya tusaidiane kumuondoa mkulima kwenye utegemezi wa mikopo ya benki na badala yake tuwaelimishe wajiwekee akiba ya kumudu pembejeo za msimu unaofuata,” alisisitiza.

Aidha Waziri Majaliwa alisema kama kutakuwa na ulazima wa kuingia kwenye mikopo, viongozi hao hawana budi kuhakikisha kuwa wanaisimamia kwa kikamilifu.

“Kama mtaingia kwenye mikopo, lazima mjipange kuisimamia mikopo hiyo ili isije ikawarudisha nyuma wakulima wetu kwenye mfumo ambao ulikuwa unawaumiza,” aliongeza.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents