Habari

Waziri Mkuu aweka wazi hali ya ukuaji wa uchumi

By  | 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Taifa unaridhisha, ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7.

Ameyasema hayo Ijumaa, wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, mjini Dodoma.

“Mwenendo wa uchumi wetu ni wa kuridhisha, kwa mfano ukuaji wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7, robo ya pili ilikuwa asilimia 7.8 na nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa ni asilimia 6.8,” alisema Waziri Mkuu.

Amesema hali hiyo inafuatia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na usimamizi thabiti wa matumizi ya Serikali, ambapo nakisi ya bajeti ya Serikali imeshuka na kufikia asilimia 1.9 kwa mwaka 2016/2017

Aidha Waziri Mkuu alisema akiba ya fedha za kigeni inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya kipindi cha miezi mitano, ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne.

Akizungumzia kuhusu kasi ya upandaji bei, Waziri Mkuu amesema takwimu zinaonyesha kwamba katika nusu ya mwaka 2017, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha tarakimu moja.

“Takwimu zinaonyesha kwamba mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Oktoba 2017 ulikuwa ni asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilima 5.3 mwezi Septemba, 2017.”

Jiunge na Bongo5.com sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Bongo5!

Add a comment

comments