Habari

Waziri Mwakyembe awafunda watumishi wa wizara ya habari

Watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wamehimizwa kutumia muda wao wa kazi kuwahudumia wananchi kwa kujibu hoja na kutatua kero zao kwa haraka na ufanisi.

Hayo yamesemwa Mkoani Dodoma na Waziri Mhe. Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akifungua kikao cha 13 cha Baraza la Wafanyakazi cha Wizara hiyo, ambacho hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za watumishi.

“Ni wajibu wa kila mtumishi kuzingatia maadili na weledi katika kuhakikisha utumishi wa umma unaheshimika na kuwajibika kwa wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa kazi zetu” amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha Dkt. Mwakyembe ameziagiza mamlaka zinazosimamia nidhamu katika Wizara hiyo kutosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wasiotimiza wajibu wao ili kuimarisha utendaji wa kazi.

“Serikali ya awamu ya tano ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha taratibu za kiutendaji zinafuatwa na kuzingatiwa” amesema Dkt. Mwakyembe.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi alimshukuru mgeni rasmi kwa kuwafungulia kikao hicho ambacho kipo kwa mujibu wa sheria, na kuwasisitiza watumishi kuyafanyia kazi yale yote waliyoelezwa.

“Nawaomba watumishi kuzingatia na kutekeleza wajibu wenu katika majukumu yenu ya kila siku,kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizoainishwa katika mikataba ya ajira” amesema Bibi.Susan.

Naye Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Bw.Makoye Alex Nkenyenge alimshukuru mgeni rasmi kwa niaba ya wajumbe wote na kuhaidi kuyafanyia kazi yale yote aliyoyaeleza katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents