Habari

Waziri Ummy atoa tamko siku ya afya ya akili duniani

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameeleza kuhusu Siku ya Afya ya Akili Duniani, ambayo huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 10 ya mwezi Oktoba ambapo kauli mbiu ya mwaka huu “Afya ya Akili Mahali pa Kazi”.

Hii ni taarifa ya Waziri Ummy kwa wananchi kuhusu madhimisho ya siku hiyo:
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka 2017 ni “Afya ya Akili Mahali pa Kazi” Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha Waajiri na watunga sera namna bora ya kuhusisha Afya ya Akili katika ngazi mbalimbali za kutengeneza miongozo ya kisera na kuifanya afya bora ya akili kuwa ni sehemu ya ustawi wa wafanyakazi.

Ndugu Wananchi,

Tanzania kama ilivyo nchi zingine wanachama wa shirika la Afya Duniani wanaadhimisha siku hii, ambapo Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa shughuli mbalimbali za kutoa elimu kuhusu umuhimu wa afya ya akili mahali pa kazi na kuwafanya waajiri na wafanyakazi kutambua umuhimu wa afya bora ya kiakili na huduma za afya ya akili.

Ndugu Wananchi,
Tunapozungumzia afya tunamaanisha hali ya ustawi wa mwanadamu kimwili, kiakili na kijamii. Mtu mwenye afya njema ya akili anaaminika kwa kutengemaa katika namna anavyofikiri, anavyohisi, na anavyotambua mambo, ambayo kwa pamoja hujionyesha katika matendo yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na jinsi anavyohusiana na kushirikiana na wenzake katika familia na jamii na mahali pa kazi kwa ujumla.

Magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri au yanapelekea mabadiliko katika kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa na mabadiliko ya kitabia au mwenendo uliotofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, desturi, na nyanja nyingine za kijamii. Tabia hizo zinatokana na ugonjwa wa akili kuathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) pamoja na kuathiri uhusiano wake katika jamii na hivyo huathiri jamii nzima inayomzunguka.

Visababishi vya magonjwa ya akili vimegawanyika katika sababu za kibaolojia, kisaikolojia na kijamii na mjumuiko wa visababishi hivi ndivyo vinavyopelekea mtu kuwa na dalili za ugonjwa wa akili.

Ndugu Wananchi,

Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinaonyesha kuwa kati ya watu wazima wanne mmoja kati yao alishapata au alishaona mtu mwenye matatizo ya kiakili, ambayo hutokana na mila na desturi zilizopitwa na wakati, unyanyasaji, unyanyapaa na kutengwa au kubaguliwa kwa namna yeyote.

Hali kadhalika hata katika nchi yetu tumekuwa tukikabiliwa na matatizo kama hayo ya mila na desturi zisizo rafiki, unyanyapaa na ubaguzi ambao unasababisha pia ufinyu wa bajeti, uhaba wa wataalamu katika vituo vya kutolea huduma, uhaba wa vifaa tiba na dawa kwa wagonjwa wenye matatizo ya kiakili, kijamii na kisaikolojia. Tunapaswa kukumbuka kuwa hakuna afya njema ya kimwili kama hakuna afya ya akili; na pia nchi yetu ikiwa na wafanyakazi wenye afya bora ya akili ni hazina kubwa kwa Taifa letu.

Ndugu Wananchi,
Katika kukabiliana na ukweli huu jitihada mbalimbali zimefanywa za kutoa huduma za afya ya akili ikiwa ni pamoja na kutengeza Mwongozo wa kisera wa afya ya akili ya mwaka, 2006 na Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008 ambavyo unatoa mwongozo wa namna ya kutoa huduma. Aidha, serikali inaendelea kuhamasisha waajiri kuwekea mkazo mambo mbalimbali ya kuimarisha huduma za afya ya akili katika mipango yao, na kuhakikisha kila Mkoa unaimarisha huduma hizi katika ngazi ya Mikoa yote Tanzania Bara.

Vilevile serikali inaendelea kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ya akili nchini ili waweze kutambua na kubaini mapema dalili za magonjwa ya akili na kutoa matibabu stahiki au rufaa kwa wakati muafaka. Pia, tumeimarisha matibabu ya magonjwa ya akili na saikolojia katika hospitali za mikoa na rufaa hii ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa afya ya akili wakiwepo madaktari bingwa na wauguzi bingwa ili kuweza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wale wa ndani/ waliolazwa.

Ndugu Wananchi,
Watu wengi wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu magonjwa ya akili, na kufikia hatua ya kuhusisha na laana, kurogwa, kuwa na mapepo au kutupiwa majini; Magonjwa ya akili ni magonjwa kama yalivyo mengine na yanaweza kumtokea mtu yeyote wa rika lolote na muda wowote, hivyo basi wananchi, wanafamilia na jamii kwa ujumla tunapaswa kujua na kutambua dalili za magonjwa ya akili na kuwasaidia kupata matibabu, kupunguza unyanyasaji, unyanyapaa na kuwatenga wagonjwa wa akili. Taarifa ya afya na magonjwa ya akili ya mwaka 2015/16 inaonyesha kuwa takribani wagonjwa 611,789 wameweza kuhudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya nchini.

Katika kukabiliana na wimbi la ugonjwa wa Afya ya akili wataalamu na waajiri wataendelea kuelimisha jamii juu ya magonjwa ya akili na kupinga vitendo vya unyanyasaji, unyanyapaa na kuwatenga wagonjwa hivyo, kuwawezesha kufikishwa maeneo ya utolewaji wa huduma na tiba mapema ili wasaidiwe kama walivyo wagonjwa wengine

Ndugu Wananchi,

Dhamira kuu ya maadhimisho ya mwaka huu 2017, ni kuhakikisha afya ya akili inakuwa sehemu ya agenda kila mwaka mahali pa kazi na kwamba waajiri na waajiriwa waweze kuweka mikakati/mipango ambayo itazuia/ itapunguza au kuondoa visababishi vya magonjwa ya akili na uwezeshaji wa utambuzi wa mapema kwa walio na dalili za magonjwa ya akili na hivyo kupatiwa tiba.

Aidha, dhamira pia inalenga kuhakikisha kuwa mahali pa kazi ni mahala salama na pasipokuwa na visababishi/vichochea/vihatarishi vinavyopelekea waajiri na waajiriwa kupata dalili za magonjwa ya akili kwa sababu ndio sehemu ambayo mwajiriwa/waajiriwa wanakaa muda mrefu kuliko muda wa majumbani.

Vilevile, dhamira inalenga kuongeza thamani, heshima na utu wa mgonjwa wa akili, kuzifanya huduma za afya ya akili kama sehemu muhimu ya huduma ya mwili wa binadamu, kupunguza unyanyapaa, kutengwa na kunyanyaswa, kuifanya jamii kuongeza uelewa na kutambua magonjwa ya akili kama magonjwa mengine na hivyo kuyapa kipaumbele.

Ndugu Wananchi,

Serikali imeendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka (2007) ambayo inalenga kutoa huduma bila malipo kwa wagonjwa wa akili na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Aidha Sera ya Mwongozo wa Huduma za Afya ya Akili inasisitiza utoaji wa huduma za Afya ya Akili bila malipo. Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kutambua uwepo wa maadhimisho ya siku ya Afya ya Akili duniani kama sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani.

Ndugu Wananchi,

Ili kuboresha hali ya afya ya akili Serikali kwa kushirikiana na wadau itahakikisha kwamba: – inaongeza uelewa wa jamii kuhusu visababishi, dalili na huduma zinazohusiana na afya na magonjwa ya akili ikiwemo:

Watumishi wa afya wanapatiwa mafunzo maalum ya namna ya kuchujua/kuchunguza dalili za magonjwa ya akili na kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa wa akili.
Kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuboresha huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa ya akili katika jamii.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents