Burudani

Wema Sepetu atinga bodi ya filamu kuomba kufutiwa adhabu kutokana na mwenendo wake mzuri (+Video)

Msanii wema Sepetu leo ametinga katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) baadhi ya maelekezo aliyopewa kuyafuata kufuatia adhabu aliyopewa tarehe 26 Oktoba mwaka huu kutokana na ukiukwaji wa Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Na. 4 ya mwaka 1976.

“Msanii  wa Tasnia ya Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini Wema Isaac Sepetu mapema leo amewasilisha katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) baadhi ya maelekezo aliyopewa kuyafuata kufuatia adhabu aliyopewa tarehe 26 Oktoba mwaka huu kutokana na ukiukwaji wa Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Na. 4 ya mwaka 1976.
Bodi ya Filamu ilimfungia kwa muda usiojulikana na kumtaka kuyafanyia kazi maeneo muhimu matatu ambayo ni kuandika kwa maneno yasiyozidi 1500 mambo yote mazuri aliyowahi kuyafanya kwenye maisha yake, aandike changamoto alizowahi kukutana nazo kwenye maisha yake na aandike ni kwa namna gani anaweza kusafisha taswira yake kutokana na matendo yake hasi aliyoyafanya.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo Alieleza kuridhishwa na mwenendo wa nguli huyo wa Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini kufuatia utiifu wake wa adhabu aliyopewa na kusema Tasnia ya Filamu bado inamuhitaji na kama akiendelea na mwenendo mzuri basi atafunguliwa kutoka kwenye adhabu aliyopewa.
“Tunamuhitaji sana Wema Sepetu katika Tasnia ya Filamu kutokana na umahiri wake katika kazi lakini tunachukia maadili mabovu aliyoyaonesha katika jamii na sisi kama Bodi ya Filamu hatutasita kumfungia moja kwa moja kama akiendelea na matendo yauvunjifu wa maadili yetu kama Watanzania.”Alisema Fissoo.
Kwa upande wake Wema Sepetu amesema anajutia sana kufungiwa kwake kutokushiriki kwenye kazi za Filamu kwakuwa anakosa fursa nyingi za kufanya kazi za kimataifa na ameahidi kuendelea na mwenendo mzuri ili aweze kuwa mfano wa kuigwa na jamii inayo mtazama, hivyo akaiomba Bodi ya Filamu ijaribu kumfikiria na kumfungulia mapema kwa kuwa anategemea kuendesha maisha yake kupitia kazi ya Filamu.
“Filamu ndio kitu ninacho kitegemea kwenye maisha yangu na tangu nimefungiwa nimekosa fursa nyingi za kazi ambazo zingetutangaza kimataifa, hivyo naahidi kuendelea kuwa na mwenendo chanya katika jamii pasipo kuharibu maelekezo niliyopewa na Bodi ya Filamu katika kuisafisha taswira yangu ambayo imechafuka”
Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Wema Sepetu kuhakikisha anarudisha Taswira yake chanya iliyopotea na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii na ikiwa mwenendo wake utazidi kuwa mzuri basi atafunguliwa kutoka kwenye adhabu aliyopewa.”

By Ally Juma.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents