Moto Hauzimwi
TECNO Spark 2

Zitto kulishitaki Bunge

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe (CHADEMA), ambaye amemaliza adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na kusema uongo bungeni, amemwandikia Spika, akilitaka Bunge lipitie upya adhabu aliyopewa.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima

 

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe (CHADEMA), ambaye amemaliza adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na kusema uongo bungeni, amemwandikia Spika, akilitaka Bunge lipitie upya adhabu aliyopewa.

 

Ingawa ameahidi kuyaheshimu maamuzi yatakayofikiwa iwapo hatua hizo zitafuatwa lakini haki isitendeke, Zitto ameonya kuwa anaweza kuchukua hatua ya kulifikisha suala hilo mahakamani, ili kuhakikisha anatetea haki yake.

 

Zitto analitaka Bunge kupitia Kamati ya Kanuni, lipite adhabu hiyo kwa kuwa anaamini kuwa haikuwa ya haki, imemuonea na kumdhalilisha mbele ya macho ya jamii ya Kitanzania na kimataifa.

 

Anaainisha maombi sita, akiamini kuwa kupitia hatua anazoliomba Bunge kuzipitia, ametoa nafasi kwa mhimili huo wa utawala kujikosoa, kujisahihisha na kujirekebisha kutokana na makosa liliyoyafanya kwa kumuadhibu pasipo kuzingatia kanuni.

 

“Mheshimiwa Spika, mimi kama mbunge katika Bunge lako, naamini ya kwamba adhabu niliyopewa ilifikiwa kwa shinikizo la kiitikadi na hata kufikia kundi moja la wabunge kutumia vibaya wingi wao bungeni (abuse of majority) na kuniadhibu bila kufuata kanuni za Bunge,” anaeleza Zitto katika barua hiyo ya kurasa nne ambayo Tanzania Daima imeiona.

 

Alipotakiwa na gazeti hili aeleze ni kwa nini ameamua kuchukua hatua hiyo hivi sasa na si kabla, Zitto alisema kuwa hakutaka kuingilia maamuzi yaliyofikiwa ndiyo maana aliamua kumaliza kuitumikia adhabu kabla ya kuchukua hatua hiyo.

 

Alisema kuwa alikuwa na uwezo wa kwenda mahakamani kutafuta haki yake lakini ameamua kuchukua nafasi hiyo ili kulipa Bunge nafasi ya kujirekebisha lenyewe.

 

“Nilikuwa na nafasi ya kwenda mahakamani na mawakili wengi walijitolea kunitetea lakini nimeona kufanya hivyo ni kuipambanisha mihimili ya utawala wakati ipo nafasi ya kulipa Bunge nafasi ya kujirudi.

 

“Nafahamu kuwa upo uwezekano kama ningekwenda mahakamani, ingeniuliza iwapo nimejaribu kufanya njia zozote za kulitatua tatizo hili nje ya mahakama… na ndivyo ninavyofanya hivi sasa, na iwapo itafikia mahali nitaona bado sijatendewa haki, nitakwenda mahakamani nikiwa na rekodi za adhabu ya awali na yatakayojadiliwa katika kamati,” alisema.

 

Aliliambia gazeti hili kuwa, kwa kuwa Bunge ni taasisi ambayo inaendeshwa kwa kanuni, anaamini kuwa safari hii litazingatia kanuni hizo na kubaini makosa yaliyofanyika ili kutoa haki.

 

Katika maombi yake sita, Zitto analiomba Bunge, kupitia Kamati ya Kanuni za Bunge, kupitia adhabu aliyopewa Agosti 14 mwaka huu na lijiridhishe kama kanuni za Bunge zilifuatwa.

 

Aidha, baada ya kupitia vifungu vyote na kumsikiliza yeye katika kikao cha kamati, Zitto analitaka Bunge lipitie kauli za viongozi wote wa Bunge na serikali kuhusu adhabu aliyopewa na kuona kama hawakuvunja kanuni za Bunge na sheria namba 3 ya mwaka 1988.

 

“Kama Bunge likiridhika kuwa matamshi ya viongozi niliowataja yanakiuka kanuni za Bunge, kwa hali yoyote ile, basi wapelekwe katika kamati husika ya Bunge,” anasema.

 

Pia, mbunge huyo kijana, anataka iwapo itabainika kuwa kulikuwa na makosa katika kumuadhibu, basi Bunge limuombe radhi kwa kumpa adhabu isivyo halali.

 

Pia analitaka Bunge lijutie maamuzi liliyoyachukua na kuahidi mbele ya jamii kuwa halitarudia kuvunja kanuni za Bunge kwa makusudi na kumuadhibu mwakilishi wa wananchi mwingine bila makosa.

 

“Bunge liahidi kuwa kamwe haitatokea mbunge kuonewa kwa sababu za kiitikadi au kukomoa na kupiga marufuku vikao vya kamati za vyama vya siasa ndani ya Bunge kupanga njama za kuadhibu wabunge bila makosa,” anabainisha Zitto katika ombi lake la sita.

 

Akieleza kwa nini anaamini kuwa dhabu hiyo haikuwa ya haki, Zitto anasema kuwa hatua za kumuadhibu hazikufuata kanuni za Bunge, hazikuzingatia tamaduni za Bunge na kubwa zaidi hazikumpa nafasi ya yeye kujitetea.

 

“Muda wa kuwasilisha hoja yangu, ambao kwa masikitiko makubwa, viongozi wa Bunge mmeuelezea kama ndio muda niliopewa kuthibitisha maneno yangu, ni muda wa kikanuni ambao niliomba mimi ili kuleta hoja binafsi na wala si muda niliopewa kuthibitisha jambo lolote,” anasema.

 

Akichanganua kanuni, Zitto anabainisha katika barua hiyo kuwa Bunge lina taratibu za kuleta hoja bungeni ambazo zimefafanuliwa kinagaubaga katika kanuni ambazo zinaanisha wazi kabisa kuwa hoja haiwezi kutolewa juu ya hoja nyingine na kwamba muda wa kutoa taarifa ya hoja umewekewa utaratibu ndani ya kanuni za Bunge.

 

“Kanuni zetu zinasema wazi kabisa (59-3) kuwa iwapo mbunge anashutumiwa kusema uongo bungeni, au kutoa lugha ya kuudhi, atapewa muda ili kuthibitisha hili analoshutumiwa.

 

“Mimi Mheshimiwa Spika, si tu sikuwahi kushutumiwa kuserma uongo, bali pia wewe binafsi unajua sijawahi kupewa muda kuthibitisha chochote,” anasema Zitto.

 

Anaongeza kuwa alisimamishwa kwa kusema uongo bungeni, lakini hajaelezwa mahala popote uongo huo ni upi.

 

“Mbaya zaidi baadhi ya viongozi wa Bunge, ukiwemo wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Katibu wa Bunge mliendelea kuonyesha kuwa dhabu ile ni sahihi na kuwaaminisha wananchi kuwa mimi ni mbunge muongo.

 

“Vile vile viongozi wa upande wa serikali, akiwemo waziri mkuu, mawaziri na manaibu mawaziri wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema mimi ni muongo kufuatia adhabu hiyo,” anasema.

 

Anasema kuwa licha ya kumdhalilisha yeye kama mtu binafsi, adhabu hiyo ni ishara mbaya sana kwa demokrasia ndani ya Bunge. Alisema angependa kuona Bunge likiheshimika na ndiyo maana akaamua kuitumikia adhabu yote na kutotoa kauli yoyote iliyoingilia mamlaka ya Bunge kuhusiana na dhabu hiyo.

 

“Mheshimiwa Spika, ombi langu hili mbele yako ni muhimu sana katika kulifanya Bunge lijiangalie na kujirekebisha, kama inabidi, pale ambapo litakuwa limekosea. Hii itasaidia kuepuka makosa kama haya siku za usoni,” anasema Zitto.

 

Agosti 14 mwaka huu, wakati wa kikao cha bajeti, Bunge lilimsimamisha Zitto kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir, akidai kuwa Zitto alikuwa amelidanganya Bunge katika hoja yake binafsi aliyoiwasilisha awali.

 

Katika hoja hiyo binafsi, Zitto alikuwa analitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini mkataba wa mradi wa mgodi wa Buzwagi nje ya nchi.

 

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao siku hiyo hiyo walipitisha azimio la kumsimamisha mbunge huyo.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW