Habari

Afariki akifanyiwa upasuaji wa tezi dume na daktari feki

Mkazi wa Singida amepoteza maisha baada ya kutokwa na damu nyingi kutokana na kufanyiwa upasuaji wa tezi dume na daktari feki.
Daktari

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, alimtaja mzee huyo aliyefanyiwa upasuaji wa tezi dume, kuwa ni Israel Shaban (68) mkazi wa kijiji cha Kinyambuli kata ya Nkinto tarafa ya Kirumi wilaya ya Mkalama.

Alisema Julai, 14 mwaka huu saa mbili usiku mzee Shaban alienda nyumbani kwa Joseph Msafiri anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40 ambaye alikuwa ameigeuza nyumba yake kuwa ni kituo cha kutolea huduma za afya.

Akifafanua, alisema inadaiwa kuwa Joseph katika miaka ya nyuma aliwahi kuwa mwajiriwa wa serikali kwa nafasi ya utabibu.

Kamanda Sedoyeka alisema kutokana na uzoefu huo, baada ya kuacha kazi serikalini, huku akijiita ni daktari, aliamua kuanza kutoa tiba ikiwemo upasuaji nyumbani kwake kinyume na sheria.

“Mtuhumiwa baada ya kumfanyia upasuaji huo wa kienyeji Mzee Shaban katika sehemu zake za siri, alitokwa damu nyingi na kupelekea kuwa katika hali mbaya. Mtuhumiwa alipobaini hali hiyo, alimtekelekeza na kufanikiwa kutoroka na kukimbilia kusiko julikana. Kwa sasa tupo kwenye msako mkali ili kumkamata na kumfikisha mahakamani,” alisema.

Aidha, alisema baada ya kufanya upekezi kwenye nyumba ya dakatari feki huyo, wamefanikiwa kukamata vifaa vingi vya utabibu na dawa nyingi za kutibu binadamu.

Source: StarTV

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents