Habari

Airpay Tanzania kusaidia noti ya Tanzania kutochakaa sokoni

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na mipango Zanzibar Dk. Saada Mkuya Salum, amesema kuwa kuzinduliwa kwa mfumo wa kufanya malipo kwa njia ya mtandao wa Airpay Tanzania utaisadia noti ya Tanzania kuwa katika mzunguko kwa muda mrefu.

Waziri Saada aliyasema hayo jana wakati akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi katika uzinduzi wa mfumo wa kampuni hiyo Airpay Tanzania uliyokwenda sambamba na uzinduzi wa Mtandao w Idara ya Mashirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) uliyofanyika hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege.

Alisema mfumo wa Airpay utaweza kusaidia kupunguza matumizi ya fedha taslimu sokoni na badala yake kutumia mtandao ambapo utasaidia kuiwezesha fedha kutokuchakaa wala serikali kutopata hasara ya kuzalisha fedha mpya kila mara.

“Mfumo huo utawasaidia wajasiriamali wadogo wadogo kutumia teknolojia ya kidigital katika kufanya malipo pamoja na utaongeza usalama wa fedha yetu,” alisema Waziri Mkuya

Hata hivyo alìsema kuwa uamuzi wa kampuni ya Airpay kuanzisha kituo cha teknolojia nchini utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Alisema mfumo huo utakuza uchumi wa nchi hasa ikizingatiwa kuwa serikali ya Zanzibar inatekeleza sera za uchumi wa bluu na inajitahidi kuweka mazingira mazuri ili kuvutia wawekezaji.

Akizungumzia ajenda ya mifumo ya digitali nchini, waziri huyo alitoa rai kwa taasisi mbalimbali za serikali kutumia mifumo ya wakala wa serikali mtandao na kuitaka taasisi hiyo kuhakikisha usalama wa mifumo inayoanzishwa ili kupunguza changamoto za kifedha.

Mwazilishi mwenza wa Kampuni ya Airpay Tanzania Yasmin Chali (kushoto) pamoja na Kamishna wa Idara ya Mashirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) Dk. Bili Kiwia (kulia) kwa pamoja wakionesha mkataba walioingia wa kufanya kazi pamoja mara baada ya kusainiwa. ( picha na mpiga picha wetu)

Aidha aliishauri kuzisaidia taasisi na mashirika ya umma kuyafikia masoko ya kidigitali ili kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kujenga utamaduni wa matumizi ya mifumo ya malipo kidigitali badala ya fedha taslimu.

“Pongezi na shukrani kwa serikali ya India kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar na Tanzania jambo linalokwenda kuimarisha zaidi uhusiano mzuri”amesema.

Alisisitiza kuwa kwa kipindi kirefu serikali ya Zanzibar ilijaribu kutafuta suluhisho kutoka katika matumizi ya fedha taslim na kwenda kulipia kimtandao ambao hakuna sababu ya kubeba fedha kwa ajili ya kununua bidhaa au kufanya malipo mbalimbali.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alisema kuwa mfumo wa malipo uliozinduliwa utachangia ukuaji wa uchumi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Alieleza kuwa mfumo huo unajumuisha makundi yote yanayohusika na biashara, ujasiriamali na uhaulishaji wa fedha na mfumo huo sio mgeni na nchi mbalimbali unatumia na lengo mahsusi serikali kuwa na takwimu halisi ya mwenendo wa uchumi.

“Katika mazingira yetu ya Zanzibar zaidi ya asilimia 70 ya wafanyabiashara bado hawajarasimishwa hivyo hakuna takwimu halisi za uchagiaji wa kodi kwa wafanyabiashara hao wakiwemo wakubwa, wakati na wadogo”amesema Soraga.

Waziri wa Biashara na Viwanda Omar Said Shabani, alisema mfumo huo wa Airpay utawezesha mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na waoa huduma katika kufanya malipo mbalimbali.

Alìsema mfumo huo utaleta mapinduzi makubwa na kuweka mazingira mazuri ya biashara, ufanyaji wa malipo na kwamba wizara yake inatarajia kufanya maonesho ya kibiashara hivyo mfumo huo utumike katika ulipaji.

Kamishna wa Idara ya Mashirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) Dk. Bili Kiwia, alisema mfumo huo wa Airpay utasaidia kurasimisha wajasiriamali, sekta isiyo rasmi na kufanya biashara kidigitali pasipo na uhitaji wa fedha taslim.

Kwa upande wake Mwazilishi mweza wa Airpay Tanzania Yasmin Chali, alisema wameamua kuwekeza Zanzibar kutokana na umahiri wake kwenye biashara na uvumbuzi wa masuala mbalimbali hivyo watajitahidi kuhakikisha uwekezaji wao unawanufaisha watu wote.

Alieleza kuwa katika kufikia lengo hilo watahakikisha wanatoa elimu ya matumizi jumuishi ya fedha ili kuwafanya wajasiriamali na watumiaji wengine wa huduma za kifedha kukua kibiashara lakini pia kupata suluhu juu ya masuala ya fedha.

Naye Mwanzilishi wa Kampuni ya Airpay, Kunal Jhunjhunwala alisema ” Lengo letu tunataka kumfikia mtuwa kawaida kabisa na kwa jinsi Zanzibar inavyoendelea tumeona ni mahali sahihi kuja kuwekeza, tunataka kutoa huduma bora katika nchi zaidi ya 12,” alisema

mwishoo…

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents