Ajali yaua 12 Gairo

AjaliJINAMIZI la ajali za barabarani liliibuka jana katika mipaka ya mikoa ya Morogoro na Dodoma na kusababisha vifo vya watu 12 na 32 wengine kujeruhiwa

na Ghisa Abby, Morogoro


 


JINAMIZI la ajali za barabarani liliibuka jana katika mipaka ya mikoa ya Morogoro na Dodoma na kusababisha vifo vya watu 12 na 32 wengine kujeruhiwa.


Miili ya marehemu, ambao hadi tunakwenda mitamboni walikuwa bado hawajatambuliwa, ilikuwa imepelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.


Majeruhi 12 walifikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kupatiwa matibabu na kuruhusiwa huku baadhi ya majeruhi wakikimbizwa Morogoro.


Ajali hiyo ilisababishwa na mabasi mawili; Happy Nation na Champion, ambayo yalikuwa yakisafiri kati ya mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.


Habari zilizopatikana kutoka katika eneo la ajali na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi, zilieleza kuwa, magari hayo yaliparuzana baada ya jaribio la basi la Champion kutaka kulikwepa lori lililokuwa limesimama kando ya barabara kushindikana.


Kilichosababisha ajali hiyo kuwa kubwa kwa kiasi hicho, kinaelezwa kuwa ni mwendo mkali ambao mabasi hayo yalikuwa yakienda.


Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 4:10, karibu na kituo cha ukaguzi cha askari wa usalama barabarani, katika eneo la Gairo wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, katika mpaka wa mikoa hiyo miwili.


Watu walioshuhudia ajali hiyo, walilieleza gazeti hili kuwa wakati Champion ilipofika eneo hilo, dereva aliyetambulika kwa jina la Haruna Ally, aliliona lori hilo likiwa pembeni mwa barabara na alijaribu kukwepesha gari lake upande wa pili, ambako basi la happy Nation lilikuwa likitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam.


Habari zinaeleza kuwa lori hilo lilikuwa limesimamishwa na trafiki ambao walikuwa wanalifanyia ukaguzi na wakati shughuli hiyo ikiendelea, basi la Champion, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma, lilitokea upande wa pili.


Inadaiwa kuwa lori hilo lilikuwa limeonyesha ishara ya kusimama na haieleweki ni kwa nini madereva wa mabasi hayo hawakuchukua tahadhari kubwa katika eneo hilo, ambalo licha ya kuwepo kwa lori lililosimama, pia kuna kituo cha ukaguzi.


Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametoa salamu za pole kwa ndugu na jamaa wa marehemu waliopoteza maisha katika ajali ya mabasi iliyotokea karibu na Gairo mkoani Morogoro jana.


Katika salamu zake hizo, Waziri Mkuu Pinda alisema alipokea kwa masikitiko habari za vifo hivyo vilivyotokana, kwa mara nyingine tena, na ajali ya barabarani na kusema lazima ipatikane dawa ya kupunguza ajali hizo.


“Natoa pole kwa ndugu na jamaa wa marehemu na inasikitisha kuwa taifa limepoteza tena maisha ya watu kutokana na ajali za barabarani. Naomba majeruhi wapone haraka,” alisema Waziri Mkuu.


 


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents