Habari

Aliyemfyeka mikono mkewe afungwa

Mwanaume anayeishi kijiji cha Ntala, Kata ya Singisa mkoani Morogoro, Adrian Chasambi (26) ambaye alimkata mikono mke wake kwa madai ya kunyimwa unyumba, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela.

Na Fitina Haule, PST Morogoro

Mwanaume anayeishi kijiji cha Ntala, Kata ya Singisa mkoani Morogoro, Adrian Chasambi (26) ambaye alimkata mikono mke wake kwa madai ya kunyimwa unyumba, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela.

 

Sambamba na kifungo hicho, pia mshtakiwa huyo aliamriwa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro kuhakikisha kwamba, anamlipa mke wake huyo fidia ya Sh. milioni moja.

Alipewa adhabu hiyo na Hakimu Emily Mwambapa baada ya mshtakiwa kukiri kutenda kosa hilo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwambapa alisema ametoa adhabu hiyo `kali`�kwa kuwa mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo kwa makusudi huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Hakimu huyo alisema adhabu hiyo itakuwa ni fundisho kwa mshtakiwa na wanaume wengine wenye tabia ya kuwajeruhi wake zao kutokana na kile kinachodaiwa kuwa na madaraka nao kwa kila jambo.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Hakimu alimpa mshtakiwa nafasi ya kujitetea ili Mahakama impe adhabu ya huruma kwa kosa lake ambapo mshtakiwa aliomba kama ikiwezekana aachiwe huru ili aweze kurudi nyumbani na kumuuguza mke wake ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Hata hivyo, Hakimu huyo alitupilia mbali ombi hilo baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa madai kuwa kitendo alichokifanya mshtakiwa ni cha kinyama sana na kuwa mwanamke huyo amepata ulemavu wa kudumu baada ya kukatwa kiganja cha mkono wa kushoto.

Awali, Mwendesha Mashtaka, Inspekta Msaidizi Salehe Kalulu alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 10, mwaka huu saa 8:00 usiku katika kijiji cha Ntala, Kata ya Singisa, Tarafa ya Bwakila Chini mkoani Morogoro.

Mwendesha Mashtaka huyo alisema mshtakiwa huyo alimjeruhi mke wake, Bi. Veronica Thobias (33) kwa kumkata kiganja cha mkono wa kushoto na kumjeruhi mkono wa kulia pamoja na kwenye paji la uso.

Alidai kuwa, mshtakiwa huyo alimkata mke wake huyo baada ya kunyimwa unyumba kwa kuwa mke wake alikuwa yuko katika siku zake.

 

Mshtakiwa huyo kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo jana na kukiri kosa hilo na Mahakama ikampa adhabu hiyo.

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents