Habari

Benki ya NMB yatoa gawio kwa Serikali la sh bilioni 15.2

Benki ya NMB imetoa shilingi 15. 2 bilioni kama gawio kwa serikali ambayo inamiliki asilimia 31.8 ya hisa zote ndani ya Benki hiyo.Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 45 ya gawio lililotolewa mwaka uliopita ambazo serikali ilipata Sh10.48 bilioni zilizotokana na faida ya mwaka 2018.


Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB – Ruth Zaipuna alisema kuwa, fedha zilizokabidhiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana katika mwaka wa fedha 2019 baada ya kuondoa gharama na kodi ambayo ilikiwa shilingi 45 bilioni.

Zaipuna amesema mbia mwingine ni Benki ya Rabo ya nchini Uholanzi ambayo imepata gawio la shilingi 16. 8 bilioni huku shilingi 16 bilioni zikienda kwa wawekezaji wengine ikiwemo taasisi za serikali. Alisema kwa mwaka 2019 licha ya benki kuwa chini ya uongozi wa mpito, lakini iliendelea kufanya vizuri na hata kipindi cha corona bado waliendelea kufanya vizuri kwani katika nusu ya mwaka wa fedha 2020 NMB wameshasajili faida ya shilingi 93 bilioni.

Kwa mujibu wa mtendaji huyo, wameshaanza mkakati wa kuinua kilimo nchini na tayari wamekopesha wakulima shilingi 800 bilioni huku wafanyabiashara wakikopa shilingi 2.2 trilioni. Nyingine ni ununuzi wa madawati 40,000 na kompyuta 1000 zilizotolewa kwa ajili ya kusaidia shule mbalimbali na kuwa wameendelea kuwa benki bora kwenye tuzo za jarida la kimataifa la Euro Money kwa miaka 8 mfululizo.


Akipokea mfano wa hundi hiyo, Waziri wa Fedha – Dk. Philip Mpango alisema kiwango kilichotolewa ni kizuri na kuna matumaini makubwa ya gawio kupanda kwa mwaka huu. Dk. Mpango aliitaja Benki ya NMB kuwa miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri zaidi. Awali Mwenyekiti wa bodi ya NMB Dk Edwin Mhede aliahidi Benki hiyo itafanya vizuri zaidi mwaka ujao baada ya kupata Afisa Mtendaji Mkuu kwani alipokuwa akikaimu hakuwa na nguvu zaidi katika maamuzi, Hivyo, wanaamini benki hiyo itaendelea kuwa imara zaidi na kuwa mfano kwa mabenki mengine nchini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents