Habari

Shule Huria ya Skillful yafanikiwa kufaulisha wanafunzi 650 kujiunga na vyuo vikuu

MWASISI wa Shule ya Sekondari Huria ya Skillful, Diodorus Tabaro amesema kuwa tangu shule hiyo ianzishe miaka 18 iliyopita imefanikiwa kufaulisha wanafunzi 650 kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali vilivyopo hapa nchini.

Tabaro ameyasema hayo wakati wa Mahafali ya 18 ya Kidato cha Sita, yaliyofanyika shuleni hapo Ukonga ambapo wanafunzi 75 wanatarajiwa kufanya mitihani ya kuhitimu.

Amesema idadi hiyo ya wanafunzi ni mbali na wale waliojiunga na vyuo kwa ngazi ya diploma au cheti na walioamua kujiajiri na kuendelea kutafuta maisha.

Tabaro amesema idadi hiyo kubwa imetokana na hali nzuri ya ufaulu wa wanafunzi wanaopita shuleni hapo ambao hakuna anayepata daraja la nne, isipokuwa kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu.

“Siri kubwa ya sisi kufanya vizuri na kupata wasomi wengi wa vyuo vikuu ni kutoa elimu bora inayomfanya mwanafunzi na mzazi wasijute kuchagua Skillful kwasababu hatutaki arudie kufeli tena mitihani,” amesema Tabaro.

Ametaja mbinu chache za shule hiyo kufanya vizuri kuwa ni walimu kuandaliwa kuwa wazazi, walimu na viongozi wa wanafunzi ili kuwasaidia wanafunzi kufikia malengo yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Allen Maximillian amesema wanafunzi hao wanahitimu kwa kusoma kidato cha sita ndani ya mwaka mmoja katika michepuo yote ya biashara, sanaa na sayansi.

“Tumekuwa na muendelezo wa matokeo mazuri ambao unachagizwa na jitihada za walimu, mazingira pamoja na nidhamu kwa walimu na wanafunzi,” amesema.

Aliongeza kuwa, mafanikio ya shule hiyo pia yanaenda sambamba na ushirikiano na serikali ambao wamekuwa wakiwasimamia bega kwa bega kuhakikisha elimu wanayotoa inakidhi vigezo.

Naye mmoja wa wahitimu hao, Derich Mushenyera, amesema wamejiandaa vyema kufanya mitihani ya mwisho ya kidato cha sita inayoanza wiki ijayo na anaamini watafaulu.

“Maandalizi yalikuwa mazuri, walimu wametufundisha mbinu za kufaulu lakini pia tumefanya mitihani ya mazoezi ya kutosha hivyo tunaamini tupo tayari kwa mitihani na kufaulu vizuri,” amesema Mushenyera

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents