Burudani

Chipukizi Bongo Movies kwa hili msimfuatishe JB

Chipukizi ninaowazungumzia hapa namaanisha waigizaji wanaoibukia (wavulana na wasichana). Ningeweza kuzungumzia waigizaji wote lakini akili yangu inaamini ili tasnia ya filamu hapa nchini ikue ni lazima tuachane kwanza na waigizaji wa sasa ambao ni kundi fulani ambalo halibadiliki, halibadiliki kwa maana mbili.

13129368_2315600621914717_1140831449_n

(1)Hawaongezeki wengine wakawika kama wao (2), halibadiliki maana halina ubunifu uigizaji wao ni ule ule siku zote, na fikra zao ni zile zile siku zote.

Kwahiyo nazungumzia damu mpya itakayokuja na utaratibu mpya,ari mpya,fikra mpya kabisa. Nazungumzia chipukizi ambao ukikuta wameandikwa kwenye gazeti,website,blog basi asilimia 70 ya kilichoandikwa humo ni shughuli yao(filamu) na 30 iliyobaki ndio mambo mengine.

Chipukizi ambao wakihojiwa kwenye redio au televisheni basi mahojiano yanachukua asilimia 70 ya kazi anayofanya na 30 ndio maisha yake binafsi.

Nazungumzia damu mpya ambayo haitaishia kufurahia kula chakula na viongozi na kupiga picha,nazungumzia damu mpya ambayo iko tayari hata kukataa hicho chakula ili maombi yao yafanyiwe kazi. Nazungumzia damu mpya ambayo haitaona sifa kuwa karibu na viongozi bali itaona sifa kwa viongozi kuwa karibu na changamoto zao kuliko kua karibu nao wao.
Kwa maelezo hayo hapo juu nadhani nitakuwa nimeeleweka kwanini ujumbe wangu nataka uende kwa chipukizi katika tasnia yetu ya filamu.

Mi ni mdau wa tasnia hii nikiwa kama mwandishi mzalishaji na muongozaji,kwa hiyo nina maslahi na tasnia hii ndio maana nimeamua kuchukua kalamu na kuandika makala hii juu ya kauli aliyoitoa muigizaji mkubwa hapa nchini Jacob Stephen alas JB.

JB ni muigizali mzuri kwa mtazamo wangu na watu wengi pia,ila hapa juzi kaongea kauli ambayo isipofanyiwa kazi au kujadiliwa kuna watu(waigizaji) wanaweza wakaenda njia siyo. Kauli hiyo alioiongea huwa napingana nayo sana kiasi kwamba kila nikipata nafasi ya kuongea na waigizaji huwa nawafafanulia suala hilo tena kwa umakini mno ili wasipotee.

Juzi hapa nilikuwa nasoma habari katika mitandao nikakuta habari inasema” JB atosa filamu tatu za kinigeria” nikavutika tena kwa shauku kusoma yaliyomo ndani. Katika kuingia ndani nikakuta JB anasema alishapewa script zaidi ya 3 za movie za Kinigeria akazikataa kwa kuwa hela ni ndogo na akaongeza kua anachotaka sasa hivi ni hela tu kama ni kwenda kimataifa ataenda kucheza Hollywood zinazooneshwa kwenye majumba ya sinema dunia nzima na si za Nigeria na kudai hayupo tayari kutengenezwa kwa sasa (kwa maana ya jina).

Hapa napingana na JB lakini ikumbukwe hapa nazungumza mawazo yangu ambayo ningependa chipukizi wayafuate na wasifuate ya JB.

Ni suala lisilohitaji ufuatiliaji sana kujua kuwa tasnia ya filamu Nigeria ni kubwa na pana kuliko yetu Tanzania. Pia Hollywood kama itataka kualika waigizaji Afrika basi baada ya South Africa ni Nigeria. Kwahiyo tukiamini mafanikio ni kutembea na sio kupaa na kama tukiamini mafanikio ni ngazi basi Nigeria inahusika kama ngazi kama unataka kufika mbali katika tasnia hii.

Suala lingine ni la hela, hili ni pana na linaweza leta mkanganyiko,ila niseme hivi labda JB yupo sahihi kusema kuwa hela aliyopewa ni ndogo, ila hatujui ni ndogo kiasi gani. Ila kwa kauli yake kua “mimi sasa hivi nataka hela ” kwa tafsiri yangu naanza kuamini kuwa ile hela inaweza kuwa haikuwa ndogo sana bali JB anajiona kuwa ni mkubwa sana(ukweli yeye sio mkubwa kwa jamii ya Afrika nzima kama wa Nigeria).

JB anapoletwa kwenye upana wa kibara(Afrika) sio mkubwa sana bado ana nafasi kubwa ya kukua. Mimi namshauri next time akipata filamu kutoka Nigeria au nchi yeyote aombe script aisome,aulizie director ni nani na pia aulizie filamu angalau tatu za huyo director atafute aziangalie,aombe atajiwe mhusika mkuu wa filamu(kama sio yeye)amjue na aangalie filamu zake japo mbili,aulizie kampuni itakayosambaza filamu hiyo ili ajue ukubwa na upana wa kampuni hiyo,aulize kampuni itakayofanya uzalishaji,aulize ni muda gani yeye atacheza filamu hiyo,na cha mwisho iwe ni hela,siku zote kinachompeleka muigizaji mbele sio hela ni filamu nzuri – usichambue hela chambua filamu.

Chipukizi wengi nimekuwa nikiwaambia kilichomfanya Kanumba afike alipokuwa sio uigizaji mzuri peke yake bali na kuipenda kazi yake na mipango thabiti. Aliitaka Hollywood lakini akaiona ni ndefu mno kuirukia na kuifikia kwani matawi yake yalikuwa juu sana akaona aanze na matawi ya karibu na mpaka mola anamchukua alikuwa kaanza kuweka miguu kwenye matawi ya karibu ili afikie ya juu na alikuwa ameshaanza kuyafikia kwa kiasi fylani.
Huwa nawasisitizia kuwa director au producer wa filamu utakayolipwa milioni 100 ujue alikuona kwenye filamu uliyolipwa milioni moja. Kwahiyo cheza kwenye filamu uliyolipwa milioni moja kama umelipwa milioni mia ili wa milioni mia akuone.

Director, studio,producer hawatakuchukua kwa hela yako ulionayo mfukoni watakuchukua kwa filamu nzuri ulizocheza.
Kuna waigizaji Tanzania ukiweka filamu zao tatu tofauti tofauti ukaangalia unagundua filamu aliyolipwa akaridhika na unajua ambayo hakuridhika na malipo.
Kutokana na maneno yale ya JB sijajua kama aliulizwa kwa nini haalikwi na wanigeria kucheza filamu zao, au alijistukia kuwa watanzania wanaweza kujiuliza kuwa mbona JB mkali ila haitwi na wanaigeria wakati waigizaji wapya kama Remmy Gallis wanaitwa?

Waigizaji chipukizi nawasihi fuateni mfano wa JB wa kuwa waigizaji wazuri,kuweni wachapakazi kama JB, kuweni na mahusiano mazuri na waigizaji wenzenu kama JB, kwa kuwa JB ni mfano wa kuigwa katika tasnia hapa nchini.

Lakini katika hili naomba msimuige kabisa na sio sasa hivi mkiwa chipukizi hapana hata mkifikia level yake muwe na njaa hasa, na sio ya fedha bali ya mafanikio kitasnia na katika mafanikio hayo hela lazima ije tena kwa wingi .
Muigizaji anayetaka kufika mbali anaweza kukataa filamu ya malipo ya milioni 10 ambayo ni filamu mbaya na akakubali filamu ya malipo ya milioni 5 ambayo ni filamu nzuri na kinyume chake.Chipukizi(underground) Kumbuka usichambue hela chambua filamu.

Makala imeandikwa na Big Fish Seka Boyi 0753 666 444

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents