Habari

LHRC latoa tamko shambulio la ofisi za Mawakili

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeeleza kushtushwa na kufedheheshwa na tukio la kuvamiwa na kulipuliwa na mabomu kwa ofisi ya mawakili wa IMMA lilolotokea usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Shirika hilo kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho Bi Hellen Kijo Simba wameeleza kusikitika kutosikia kauli ya serikali kulaani kitendo hicho kilichotokea.

Soma taarifa kamili:

TAMKO KUHUSU SHAMBULIO DHIDI YA OFISI YA MAWAKILI YA IMMMA NA HALI YA HAKI YA UWAKILISHI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeshtushwa na kufedheheshwa na tukio la kuvamiwa na kulipuliwa na mabomu kwa ofisi ya mawakili wa IMMA lilolotokea usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti 2017 hapa Dar es Salaam, barabara ya umoja wa mataifa. Tunatoa pole kwa uongozi na watendaji wa IMMMA, wateja wao na tasnia nzima ya sheria nchini.

Kwa masikitiko makubwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu tulipokea taarifa za kushambuliwa kwa Ofisi ya Mawakili ya IMMMA, ikiwa ni sambamba na tukio la kutekwa nyara kwa walinzi wa kampuni hiyo.Watu waliofanya kitendo hicho inasemekana walikuwa wamevaa sare za jeshi la polisi.

Tukio hilo limeibua hofu kubwa katika tasnia nzima ya sheria, hususani kwa mawakili, katika kutekeleza majukumu yao.Kwa ujumla, tukio hilo ni la kikatili na la kigaidi ambalo linapaswa kukemewa na kupingwa vikali na wadau wote wa haki za binadamu, ikiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.Kwa pamoja, tunalaani vikali shambulio hilo ambalo limehatarisha maisha na kusababisha uharibifu wa mali za wakazi wa eneo hilo pamoja na Ofisi ya Mawakili ya IMMMA.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na wadau wengine wa haki za binadamu, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),TANLAP,WiLDAF, kukemea na kulaani vikali tukio hilo, ambalo linahatarisha utetezi wa haki ya uwakilishi na uwezo wa wanasheria kutekeleza majukumu yao bila vitisho. Kanuni ya 16 ya Kanuni za Msingi za Umoja wa Mataifa juu ya Wajibu wa Wanasheria za 1990 (UN Basic Principles on the Role of Lawyers 1990) inasema kwamba Serikali zitahakikisha kwamba wanasheria wanatekeleza majukumu yao bila vitisho, vikwazo au kuingiliwa kinyume na sheria. Pia, Kanuni hiyo inakataza wanasheria kutishiwa kushtakiwa au kuwekewa vikwazo vya kiuchumi au kiutawala pale wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kikazi.

Vilevile, ripoti iliyotolewa na taasisi ya The Law Society Charity ya nchini Uingereza kuhusu utawala wa sheria ya Januari 2012 inaonyesha kwamba miongoni mwa viashiria vya upotevu wa utawala wa sheria ni kuminya wanasheria. Viashiria hivyo ni pamoja na:
• Kuwepo kwa utawala wa matamko;
• Usajili wa wanasheria na kuminywa kwa chama cha wanasheria na kukifanya chama cha wanasheria kuwa ni taasisi isiyo na nguvu zozote isipokuwa ni taasisi tu yakujitolea;
• Kuwalenga wanaokosoa utawala/Serikali;
• Kuwa na hukumu tofauti kwa makosa yanayofanana (double standards);
• Kuwa na viongozi wanaokaimu kwenye ngazi za utoaji haki; na
• Kutokuwepo uhuru wa habari kwa vyombo vya habari vya taifa na binafsi.
Ikumbukwe kwamba katika kipindi kisichozidi miaka miwili iliyopita kumekuwa na matukio kadhaa ya kuwashambulia na kuwatishia wanasheria pale wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao. Mnamo mwezi Julai 2016, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya JinaiZanzibar (DDCI), Kamishna Msaidizi wa Polisi Salum Msangi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba wanasheria wanaotetea wahalifu wataunganishwa na wahalifu hao katika makosa waliyoyatenda ili ‘wakateteane wenyewe huko ndani watakapokwenda.’Kaulihii ilikemewa vikali na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, pamoja na wadau wengine, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS). Majibu yaliyotolewa na Jeshi la Polisi ni kwamba kilichosemwa na Kamisha Msaidizi wa Polisi ni ‘kuteleza tu kwa ulimi’, na hakukuwa na tamko rasmi la jeshi hilo kurekebisha kauli hiyo na kuomba radhi.

Hata hivyo, siku kadhaa ndani ya mwezi huo huo wa Julai 2016, mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wakili Shilinde Ngalula, alikamatwa na kuwekwa ndani kinyume na sheria na askari polisi Wilaya ya Ngorongoro tarehe 25/7/ 2016 akiwa kazini wilayani humo.
Kauli ya Mh. Rais ya tarehe 2 /2/2017 akiwa mgeni rasmi Siku ya Sheria ambapo pamoja na mambo mengine alitoa kauli mbaya inayoingilia Mhimili wa Mahakama na kuagiza watuhumiwa wa ujangili kuchukuliwa hatua punde wanapo kamatwa pasipokujali utaratibu wa mahakama na kuwajumuisha mawakili wote watakao watetea.

Sambamba na hilo, mnamo mwezi Machi mwaka 2017, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria alitishia kufuta Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Kauli hii ilitolewa na Mh. Harrison Mwakyembe, ambaye sasa ni Waziri wa Habari na Michezo, alipokutana na ugeni toka TLS, ambapo alisema kwamba ‘Serikali haiwezi kuona TLS ikijiingiza katika siasa’ na kama wanachama wake wanataka siasa basi Serikali haitasita kuifuta Sheria ya TLS ambayo inaanzisha chama hicho.

Katika kuendeleza hilo wizara ya katiba na sheria ilisambaza bango kitita liloleta pendekezo la kuanzisha bodi ya kusimamia na kusajili shughuli zote za mawakili na hivyo kuiondolea TLS mamlaka ya uratibu.

Tukio jingine linaloashiria kuminywa kwa uhuru wa wanasheria na haki ya uwakilishi ni kutishiwa kwa Wakili Fatma Karume mbele ya Mahakama wakati akiwa katika shughuli za utetezi wa mteja wake Tundu Lisu katika viunga vya Mahakama ya Kisutu tarehe 27/7/2017.Pia, tarehe 22/8/2017 alikamatwa Mh. Tundu Lissu wakati akitekeleza majukumu yake katika Mahakama ya Kisutu.

Jumuia ya watetezi wa haki za binadamu imepatwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama na ulinzi wa haki za binadamu nchini, ikiwemo uminywaji wa uhuru wa wanasheria na haki ya uwakilishi. Hivyo tunatoa mapendekezo yafuatayo:
1. Serikali, kupitia Jeshi la Polisi, kuhakikisha watu ambao wamehusika na shambulio la Ofisi ya Mawakili ya IMMMA wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria haraka iwezekanavyo;
2. Tasnia ya sheria iachwe huru katika kufanya kazi zake na kupatiwa ulinzi kwa mujibu wa sheria. Wanasheria waachwe watekeleze majukumu yao bila kuingiliwa wala kutishiwa. Uhuru wa wanasheria ni haki ya msingi ambayo pia ni muhimu kwa haki ya wananchi na watu wengine kuwakilishwa kisheria;
3. Mahakama, kama mhimili muhimu katika usimamizi wa haki, ina wajibu wa kuhakikisha kwamba maofisa wote wanaofanya kazi chini ya mhimili huo wanakuwa salama na wanalindwa kwa mujibu wa sheria katika kutekeleza majukumu yao. Kwa mantiki hiyo, tunamtaka Kaimu Jaji Mkuu kukemea hadharani mashambulizi dhidi ya Mhimili wa Mahakama na tabia ya kuingilia uhuru wa mhimili huo;
4. Tunamtaka Mh. Rais ateue Jaji Mkuu kwa mujibu wa Katiba, ili kuimarisha mhimili wa mahakama na utawala wa sheria;
5. Viongozi wa Serikali na vyombo vyake wenye dhamana ya kulinda usalama wa watu nchini na haki za binadamu kwa ujumla wawajibike au kuwajibishwa mara moja pale ambapo wameshindwa kusimamia ipasavyo majukumu yao; tunasikitika kuwa mpaka leo hii hatujasikia kauli rasmi ya Serikali kulaani kitendo hiki;
6. Wananchi kuwa mstari wa mbele kuripoti matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu, na uhalifu, ikiwemo mauaji mbalimbali yenye utata kwa vyombo vya dola na vituo vya kutetea haki za binadamu bila woga. Jukumu la kulinda haki za binadamu ni letu sote, sio la wanasheria, watetezi wa haki za binadamu, maafisa wa vyombo vya dola au viongozi katika ngazi mbalimbali pekee;
7. Mwisho tunatoa wito kwa wananchi wote wenye mapenzi mema,wakiwemo mawakili, wakemee vitendo kama hivi kwani vinaathari kwa kila mmoja wetu
Hitimisho
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na wadau wengine wa haki za binadamu, tunapatwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mwenendo wa hali ya haki za binadamu nchini, kutokana na matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakitokea kama ilivyoanishwa hapo juu, ambayo hayajapatiwa majibu au ufumbuzi. Je, tuko salama?
Ulinzi wa haki za binadamu, ikiwemo haki ya usalama, unatia mashaka na Serikali inahitaji kuchukua jitihada za dhati kuimarisha ulinzi wa haki hizo. Matukio ambayo yamekuwa yanatokea lazima yapewe uzito unaostahiki kwani hali ikiendelea hivi tutajikuta siku tunapoteza hadhi yetu ya “kisiwa cha amani.”Tukumbuke hakuna nchi duniani iliyoingia kwenye hali kama hizi ikabaki salama.

Imetolewa na:
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents