Fahamu

Licha ya janga la Corona, hawa ndio matajiri 10 ambao pato lao limeongezeka mara dufu

Janga la Covid -19 limefanya watu tajiri duniani kuendelea kuwa matajiri lakini limesababisha watu wengi kuishi katika umaskini, kulingana na shirika la misaada la Oxfam.

Watu wenye mapato ya chini zaidi duniani walichangia vifo 21,000 kila siku, ripoti yake inadai.

Lakini watu 10 tajiri zaidi duniani wameongeza maradufu utajiri wao wa pamoja tangu Machi 2020, Oxfam ilisema.

Oxfam kwa kawaida hutoa ripoti kuhusu ukosefu wa usawa duniani mwanzoni mwa mkutano wa Kiuchumi Duniani huko Davos.

Kongamano hilo kwa kawaida hushuhudia maelfu ya viongozi wa makampuni na kisiasa, watu mashuhuri, wanakampeni, wanauchumi na waandishi wa habari wakikusanyika katika eneo la mapumziko la Uswizi kwa ajili ya mijadala ya jopo, karamu za vinywaji na ushawishi.

Hatahivyo kwa mwaka wa pili mfululizo, mkutano huo (uliopangwa wiki hii)utafanyika mtandaoni baada ya kuzuka kwa aina mya ya corona ya Omicron ambayo imeathiri mipango ya kufanyika kwa mkutano wa watu kuhudhuria ana kwa ana.

 

Majadiliano ya wiki hii yatajumuisha hali ya ya baadaye ya janga hili, usawa wa chanjo na mpito wa nishati.

Danny Sriskandarajah, mtendaji mkuu wa Oxfam GB, alisema shirika hilo la misaada linatoa ripoti yake ya kila mwaka sanjari na kongamano la Davos ili kuvutia umakini wa wasomi wa kiuchumi, biashara na kisiasa.

“Mwaka huu, kinachotokea ni nje ya kiwango,” alisema. “Kumekuwa na bilionea mpya aliyeundwa karibu kila siku wakati wa janga hili, wakati asilimia 99 ya idadi ya watu duniani wanakabiliwa na hali mbaya zaidi kwa sababu yamasharti yaliyowekwa kudhibiti maambukizi ya virusi, biashara ya chini ya kimataifa, utalii mdogo wa kimataifa, na kutokana na hilo, watu milioni 160 zaidi wamesukumwa katika umaskini.”

Kulingana na takwimu za Forbes zilizotajwa na shirika hilo la maaada, watu 10 tajiri zaidi duniani ni: Elon Musk, Jeff Bezos, Bernard Arnault na familia, Bill Gates, Larry Ellison, Larry Page, Sergey Brin, Mark Zuckerberg, Steve Ballmer na Warren Buffet.

Ingawa kwa pamoja utajiri wao ulikua kutoka dola bilioni 700 hadi dola trilioni 1.5, kuna tofauti kubwa kati yao, huku utajiri wa Bw Musk ukiongezeka kwa zaidi ya asilimia 1,000%, utajiri wa Bw Gates’ uliongezeka kwa wastani wa asilimia 30.

Ripoti ya Oxfam inatokana na data kutoka kwa Orodha ya Mabilionea ya Forbes na ripoti ya kila mwaka ya Credit Suisse Global Wealth, ambayo inatoa usambazaji wa utajiri wa kimataifa kuanzia 2000.

Utafiti wa Forbes unatumia thamani ya mali ya mtu binafsi, hasa mali na ardhi, ukiondoa madeni, ili kubaini kile “anachomiliki”. Data haijumuishi mishahara au mapato.

Mbinu hiyo ilikosolewa hapo awali kwani ina maana kwamba mwanafunzi mwenye deni kubwa, lakini mwenye uwezo mkubwa wa kupata mapato, kwa mfano, atachukuliwa kuwa maskini kulingana na vigezo vilivyotumika.

Oxfam pia inasema kwamba kutokana na ukweli kupanda kwa bei wakati wa janga hili, imejirekebisha ikizingatia mfumuko wa bei kwa kutumia data ya Bei ya Watumiaji wa Marekani (CPI), ambayo inafuatilia jinsi gharama ya maisha inavyoongezeka kwa wakati.

Ripoti ya Oxfam, ambayo pia ilitokana na data kutoka Benki ya Dunia, ilisema ukosefu wa huduma za afya, njaa, unyanyasaji wa kijinsia na kuharibika kwa hali ya hewa kulichangia kifo cha mtu mmoja kila sekunde nne.

Ilisema watu milioni 160 zaidi walikuwa wakiishi chini ya dola 5.50 swa na (£4.02) kwa siku kuliko hali ilivyokuwa bila athari za janga la Covid.

Benki ya Dunia hutumia dola 5.50 kwa siku kama kipimo cha umaskini katika nchi zenye kipato cha kati.

Ripoti hiyo pia inasema:

  • Janga hilo linalazimisha nchi zinazoendelea kupunguza matumizi ya kijamii huku deni la kitaifa likiongezeka
  • Usawa wa kijinsia umerejeshwa nyuma, huku kukiwa na wanawake milioni 13 kazini ambao ni wachache kuliko mwaka 2019 na zaidi ya wasichana milioni 20 wakiwa katika hatari ya kutorejea shuleni.
  • Makundi ya makabila madogo yameathiriwa zaidi na Covid, wakiwemo Wabangladeshi wa Uingereza na jamii ya Wamerekani weusi.

“Hata wakati wa msukosuko wa kimataifa mifumo yetu ya kiuchumi isiyo ya haki inafanikiwa kutoa hali nzuri kwa matajiri, inashindwa kuwalinda maskini zaidi,” Bw Sriskandarajah alisema.

Alisema viongozi wa kisiasa sasa wana fursa ya kihistoria ya kuunga mkono mikakati dhabiti ya kiuchumi ili “kubadilisha mifumo mobaya tuliyo nayo”.

Hatua hiyo inapaswa kujumuisha taratibu za ushuru zinazoendelea zaidi, ambazo hutoza ushuru wa juu zaidi kwa mtaji na utajiri, na mapato yanayotumika katika “huduma bora ya afya kwa wote na ulinzi wa kijamii kwa wote” Bw Sriskandarajah alisema.

Oxfam pia inataka haki miliki kwenye chanjo za Covid-19 ziondolewe ili kuwezesha uzalishaji mkubwa na usambazaji wa haraka.

Mapema mwezi huu rais wa Benki ya Dunia, David Malpass, alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa ukosefu wa usawa duniani, akisema athari za mfumuko wa bei na hatua za kukabiliana na uwezekano huo zinaweza kusababisha uharibifu zaidi kwa nchi maskini.

Chanzo BBC.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents