Habari

Mh. Mbowe afunguka mazito baada ya kuharibiwa mali zake na Serikali

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe leo amethibitisha kuharibiwa kwa miundombinu ya shamba lake na viongozi wa serikali ya wilaya ya Hai huku akidai anajua yote hayo yanafanyika kutokana na misimamo yake ya kisiasa na kudai hawawezi kumbadili.

Tokeo la picha la freeman mbowe
Mh. Freeman Mbowe

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mbowe amethibitisha taarifa hizo kwa akisema siku ya alhamisi ya tarehe 7 mwaka huu walipokea barua kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa  Mazingira (NEMC) ambayo ilikuwa inadai kilimo wanachofanya kilikuwa kinaharibu mazingira hivyo hawapaswi kuendelea na kilimo hicho.

“Ni kweli nimepata taarifa ya kuwa mkuu wetu wa wilaya ya Hai, akiambatana na askari wa mgambo akiambatana na watu wengine ambao sijaweza kuwafahamu wakiwemo vile vile waandishi wa habari, walikwenda kwenye mradi wetu wa Kili Vegies ni mradi wa kilimo cha kisasa cha mboga mboga (Green house), tukilima mboga na matunda, tukilima mboga kwa sababu ya ‘local market’ na wakaanza kuharibu miundombinu, ikiwemo kuharibu ‘Green houses’, kukatakata mabomba , kuharibu mimea na uharibifu mwingine mwingi” ameandika Mbowe huku akiendelea kufafanua tukio hilo.

“Ni kweli tulipokea barua ya NEMC siku ya Alhamisi tarehe 7, iliandikwa tarehe 7 lakini tuliipata tarehe 8, tulijibu hiyo hoja ya NEMC, kwamba tunaamini wamekosea sheria kwa sababu kilimo chetu hakiharibu mazingira wala shutuma zilizotolewa kwamba ni kwenye chanzo cha maji sio kweli, wanadai kwamba shamba hilo limeanzishwa kwenye chanzo cha mto Weruweru jambo ambalo sio kweli, mto unaoitwa Weruweru unaanzia mlimani kabisa National Park Kilimanjaro.” 

Mbowe anasema kitendo hicho kilichofanywa na viongozi hao ni kitendo cha kufedhehesha na cha kukatisha tamaa hivyo anasikitishwa sana na kitendo hicho, huku akisema anatambua kuwa yote hayo anayofanyiwa ni kutokana na misimamo yake kisiasa, na misimamo ya chama anachokiongoza.

“Najua haya yanatokea kwa sababu ya misimamo yangu ya kisiasa kwa sababu wa muelekeo wangu wa kisiasa na uthabiti na uimara wa chama ninachokiongoza, sasa mimi siwezi kuwa kondoo, nimesema siku zote, haya mambo ya duniani anayeyalipa ni Mungu,hawatabadilisha mawazo yangu kwa kuharibu mali zangu, wanaweza kuharibu zote hata wakitaka roho yangu waichukue, waichukue tu lakini haitanisababisha nibadili msimamo wangu katika kuamini ninachokisimamia, ninachokipigania katika Taifa” ameandika Mbowe kwa kusisitiza.

Mwenyekiti huyo wa CHADEMA amesema kuwa hakuna wingi wa mali zake zinaweza kuharibiwa zikamfanya yeye akapige magoti kama watu wengine wanavyofanya, anadai yeye hawezi kupiga magoti bali atasimama kwenye ukweli na haki siku zote.

Hakuna wingi wa mali ambao wataharibu utakaonifanya Mbowe nikapige magoti kama wengine wanavyopiga magoti, sitapiga magoti, nitasimama katika kweli na haki wakati wote wa maisha yangu, kwa hiyo hili halinishangazi kwa sababu najua gharama ya ninachokilipa, wako watu wengi wamenipigia simu wakijaribu kunipa pole kunitia moyo, wengine wamejaribu kunitia hofu, wakiniambia Mwenyekiti Mbowe pengine uachane na siasa, nimewaambia sitoachana na siasa, nitafanya siasa, ilimradi ni siasa safi zenye kusimamia ukweli na haki nitasimama nazo.“ameandika Mbowe.

Hili ni tukio la pili kwa mwaka huu kutokea kwenye shamba hilo, mwezi wa kwanza mwaka huu serikali ilimtaka kiongozi huyo kusimamisha kilimo kwenye shamba hilo ikidai kuwa lipo kwenye chanzo cha maji.

Tazama picha za uharibifu wa shamba hilo

Image may contain: plant and outdoor

Image may contain: plant, tree and outdoor

Image may contain: plant and outdoor

Image may contain: plant

Image may contain: plant, tree and outdoor

Image may contain: plant, tree and outdoor

 

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents