Habari

Serikali kuboresha sheria na sera ya Miliki Ubunifu

Serikali imesema kuwa inaendelea kuboresha sheria na sera ya Miliki Ubunifu ili kuhakikisha  yanakuwepo mazingira rafiki yenye tija kwa wabunifu na Taifa kwa ujumla.

Aidha imeweka wazi kuwa Miliki Ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuendeleza na kukuza uchumi na biashara nchini.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma (Mwana FA) wakati wakati alipomuwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji katika maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu duniani  yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Mwana FA amesema ubunifu ni nyenzo muhimu katika kukuza na kuendeleza biashara, uboreshaji wa sera utaondoa changamoto na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja nchini.

Amesema serikali inauhakika Miliki Ubunifu itaondoa changamoto na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja nchini.

“Serikali imeshaweka mazingira bora na wezeshi katika suala zima la biashara kwa kutumia Miliki Ubunifu kwani tunaamini maendeleo ya nchi yanategemea Miliki Ubunifu kwa ukuaji wa uchumi,” amesema Mwinjuma.

Ameongeza kuwa serikali kwakushirikiana na Taasisi nyingine itawezesha ukamilikaji wa sera ya Miliki Ubunifu ambayo italeta mwanga katika kusimamia mwongozo wa Haki Miliki Tanzania.

Hata hivyo, Mwinjuma amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na BRELA katika kuwaimarisha wafanyabiashara na wenye makampuni kutekeleza shughuli zao za kimaendeleo.

“Tutahakikisha ifikapo mwaka 2030 kunakuwa na uwiano wa maendeleo duniani kwa kutumia Miliki Ubunifu,” amesema Mwinjuma.

Awali Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema masuala ya ubunifu yatasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.

Amesema hivi sasa wana mpango wa kuanzisha programu ya Miliki Ubunifu katika vyuo vyote nchini lengo ni kuendeleza ubunifu.

Nyaisa amesema nchi nyingi zinaendelea duniani kwa sababu ya kueneza miliki bunifu sehemu mbalimbali ndani ya nchi zao.

Mwenyekiti wa bodi ya ushauri BRELA, Profesa Neema Mboya amesema Maadhimisho hayo ni muhimu kuendelea kushereherekewa nchini kwani yanatoa fursa ya kukutanisha wadau mbalimbali na kuweza kujadiliana, kujifunza na kupata fursa ambazo zitasaidia kukuza bunifu za wabunifu nchini.

Amesema kufuatia maboresho yanayofanywa ndani ya BRELA yamepelekea kupokea wageni wengi kuja kujifunza wakiwemo Burundi pamoja na Sudan kusini.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents