Mishahara mipya yaanza kuzua balaa

Siku moja baada ya Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Bw. John Chiligati, kutoa tamko la serikali la kuwashughulikia waajiri watakaoshindwa kulipa mishahara mipya katika sekta binafsi, kampuni ya usafirishaji mizigo ya Lalji Kanji ya jijini Dar es Salaam, imepunguza wafanyakazi 120.

Na Selemani Mpochi



Siku moja baada ya Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Bw. John Chiligati, kutoa tamko la serikali la kuwashughulikia waajiri watakaoshindwa kulipa mishahara mipya katika sekta binafsi, kampuni ya usafirishaji mizigo ya Lalji Kanji ya jijini Dar es Salaam, imepunguza wafanyakazi 120.


Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Bw. Bakari Nyoni, alidai kuwa, wamepunguzwa kazi na mwajiri wao huyo na kuwalipa Sh. 100,000 kila mmoja bila kujali wameitumikia kampuni kwa muda gani.


Bw. Nyoni, alisema wafanyakazi walikuwa wanalipwa Sh. 48,000 ikiwa ni kima cha chini cha mshahara kabla ya kupandishwa na serikali.


Wafanyakazi hao walidai kuwa, waliitwa na mwajiri wao jana asubuhi na kutakiwa kila mmoja kusaini hundi iliyokuwa na kiasi cha Sh. 100,000 tu ikiwa ni malipo ya mkono wa kwa heri.


Hata hivyo, walipohoji kwa nini wanalipwa kiasi hicho cha fedha, walijibiwa na mwajiri wao kuwa kama hawataki kuchukua fedha hizo mlango upo wazi waondoke.


“Tulipohoji kwa nini wanatupa kiasi hicho cha fedha walitujibu kuwa yeyote asiyetaka kuchukua fedha hizo aondoke na hakukuwa na maelezo zaidi,“ alisema Bw. Nyoni.


Tangazo lililobandikwa na uongozi wa kampuni ya Lalji Kanji, lilisomeka “Hii ni kuwafahamisha rasmi kwamba baada ya majadiliano nanyi wafanyakazi wote,viongozi wa vyama vya wafanyakazi na kutokana na nyongeza za kima cha chini cha mishahara kilichotangazwa na serikali, tunawafahamisha rasmi kwamba baadhi ya wafanyakazi watapunguzwa kazi kutoka tarehe 31 Desemba.


Ni muhimu kwa wafanyakazi wote mkaenda katika ofisi zenu za Mbeya ama Dar e s Salaam ili kujua kuwa kama nawe utapunguzwa kuweza kupewa malipo ya haki zako.“


Kwa mujibu wa wafanyakazi hao, baadhi yao walihamishiwa jijini Dar es Salaam wakitokea Mbeya na hawakulipwa fedha za uhamisho na wamekuwa wakiishi ndani ya yadi ya magari hayo kutokana na kutokuwa na fedha za kupanga chumba.


Wafanyakazi waliopunguzwa waliitumikia kampuni hiyo kati ya miaka mitatu hadi saba na bila kujali muda waliotumikia kampuni hiyo wamelipwa fedha sawa.


Hata hivyo, juhudi za gazeti hili kutaka kupata ufafanuzi wa madai ya wafanyakazi hao waliopunguzwa kutoka kwa uongozi wa kampuni hazikufanikiwa baada kujibiwa na mlinzi aliyekuwa zamu kuwa hawakuwa tayari kuongea kwa kuwa ilikuwa ni siku ya mapumziko.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents