Habari

Mpango aitaka bodi ya NIT kuhakikisha ndege za mafunzo zinatunzwa

MAKAMU wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango ameielekeza Bodi ya Uongozi ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuhakikisha ndege za mafunzo zilizonunuliwa na serikali kwa fedha nyingi zinatunzwa vizuri na kuzingatia masuala ya usalama.

Mpango ameyasema hayo leo mkoani Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya ndege mpya Boeing 737 Max 9 na kukabidhi ndege mbili za mafunzo kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Amesema ili kuongeza ufanisi wa NIT katika kutoa mafunzo ya urubani mwezi Juni mwaka huu Serikali imewezesha chuo hicho kuingia mkataba wa ununuzi wa ndege moja mpya ya mafunzo yenye injini mbili.

“Ndege hiyo inatarajiwa kuwasili katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha ujao 2024/2025, niielekeze bodi ya uongozi wa NIT hakikisheni mnazitunza ndege hizi ili ziweze kutumiwa na wanafunzi wengi Zaidi katika mafunzo,” amesema

Naye Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema gharama ya kusomea Urubani nje ya nchi ni kubwa hivyo ni moja ya kikwazo cha kupata marubani wengi hapa nchini.

“Gharama ya kusoma urubani nje ya nchi ni Sh. Milioni zaidi ya 300 hivyo watanzania wengi hawawezi kumudu gharama hiyo, ujuio wa ndege hizi mbili za mafunzo zitawezesha mafunzo hayo kutolewa hapa nchini kwa gharama za Sh. Milioni 74,” amesema Prof. Mganilwa

Aidha amesema ndege hizo mbili mpya walizopatiwa na Serikali kila moja inauwezo wa kubeba watu wanne na zitatumika kutoa mafunzo ya awali na ya biashara.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents