Habari

Mrundikano makontena – Bandari iko hoi

MRUNDIKANO wa makontena sasa ni dhahiri umeilemea Mamlaka ya Bandari (TPA), kiasi cha kusababisha usumbufu mkubwa kwa wenye meli, wasafirishaji na waagizaji wa mizigo kutoka na kwenda nje ya nchi.

na Ratifa Baranyikwa

 

 

 

MRUNDIKANO wa makontena sasa ni dhahiri umeilemea Mamlaka ya Bandari (TPA), kiasi cha kusababisha usumbufu mkubwa kwa wenye meli, wasafirishaji na waagizaji wa mizigo kutoka na kwenda nje ya nchi.

 

Hali hiyo ya mambo imesababisha muda wa makontena kukaa bandarini kuongezeka, kutoka wastani wa siku 10 hadi kufikia siku 24 hivi sasa, kiwango kinachokaribia kuwa sawa na mwezi mmoja.

 

Aidha, ushahidi wa kulemewa huko kwa Bandari ya Dar es Salaam inayohudumia takriban mikoa yote nchini na nchi za maziwa makuu zikiwamo Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda, ni kuendelea kuzidiwa nguvu kwa Kitengo cha Makontena cha TICTS.

 

Taarifa rasmi za TPA zinaonyesha kuwa TICTS ambayo yadi zake zina maeneo yenye uwezo wa kubeba makontena 7,500 yenye urefu wa futi 20, hadi kufikia juzi Jumanne ilikuwa na makontena 8,300 kutoka 11,000 ya awali.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Jason Rugaihuruza, akionekana waziwazi kupata shida kueleza kile kinachotokea bandarini, alisema moja ya sababu ya mrundikano huo ni kubainika kwa makontena yapatayo elfu mbili ambayo yalishindikana kupakuliwa kutokana na kukosekana kwa nyaraka zake.

 

Rugaihuruza aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kulemewa huko kumeilazimisha mamlaka yake kuanzisha mpango mwingine wa dharura ulioanza kazi Ijumaa iliyopita.

 

Alisema mpango huo wa dharura ambao kimsingi unaonyesha kuanza kwa jitihada mpya za kuinusuru bandari, unawashirikisha wadau wengine ambao ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Uondoshaji Mizigo (TAFFA), Wakala wa Meli (TASAA), Wakala wa Barabara (TANROADS), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu, Anga na Majini (SUMATRA) na Wakala wa Vituo vya Kuhudumia Makontena (ICDs).

 

Mpango huo mpya kwa mujibu wa meneja huyo, unawataka wadau wote pamoja na mambo mengine, kufanya kazi kwa saa 24 na kuongeza kasi ya upakuaji, mkakati ambao unarejea wito uliopata kutolewa mwaka jana na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo.

 

Rugaihuruza alisema kuwa, pamoja na hatua mbalimbali kuchukuliwa siku zilizopita, kasi ya uondoshaji wa makontena bandarini iliendelea kuwa chini ya makontena 300 kwa siku, idadi ambayo ni ndogo sana inapolinganishwa na makontena yaliyopo kwenye yadi na yale yanayopakuliwa kutoka kwenye meli.

 

Alisema kuwa, kupitia kikao chake na wadau mbalimbali alichokifanya hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Miundombinu, Omari Chambo, aliteua kamati ya mpango wa dharura ya kuhakikisha kila mdau anatekeleza mpango huo, ikiwa chini ya uenyekiti wa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam.

 

Alisema kuwa mpango huo mpya wa dharura mbali na kuwashirikisha wadau wote wa bandari, pia umehusisha kuongezwa kwa geti la pili (namba 8), ambalo litakuwa likitumika kupitisha makontena kwa saa 24 kama ilivyokuwa kwa geti namba 5, lililokuwa likitumika awali.

 

Mbali ya hilo, alisema kuwa TRA imelazimika kuanzisha vituo vya kuhudumia makontena nje ya bandari (ICDs) ambako baadhi ya makontena kutoka TICTS yatapunguzwa kwenda huko, sambamba na kitengo cha makontena na wakala wa meli kuongeza kasi ya kutoa kipaumbele kwa makontena kwenda Tanga na Zanzibar.

 

Alisema Jeshi la Polisi litashiriki katika kusindikiza malori ya makontena kwenda ICDs.

 

Alisema kuwa uamuzi wa sasa utakuwa makontena yote yatakayopakuliwa yatapelekwa kwenye ICDs ambazo nazo zina uwezo wa kupokea makontena 7,500, na mpaka sasa makontena yaliyopo ni 4,296, wakati uwezo uliobaki wa kupokea ni makontena 3,204.

 

Hata hivyo alisema kuwa wateja wote ambao watachukua makontena kutoka ICDs hawatalipa gharama za kuhamishiwa makontena yao kutoka TICTS.

 

“Lengo ni kufikia idadi ya chini ya makontena 7,500 (ya futi 20) ambayo ndio uwezo wa kuhifadhi makontena katika kitengo cha TICTS. “Makontena kwenye yadi yatakapofikia chini ya makontena 6,200, vifaa ndani ya TICTS vitafanya kazi kwa ufanisi na haraka zaidi,” alisema.

 

Hata hivyo akizungumzia chanzo na tatizo la msongamano huo, meneja huyo wa bandari alisema kuwa, tatizo halisababishwi na mtu mmoja, bali pande mbalimbali zinazohusika na upakuaji wa mizigo bandarini.

 

“TRA ana muda wake wa kufuatilia taratibu zake, unaweza ukakuta TRA amekusainia nyaraka zako, tatizo linaweza kuwa labda TICTS huko ukakuta bado hujakamilisha taratibu zake, sasa utaratibu mpya ni wadau wote kufanya kazi kwa saa 24 na kwa wakati.

 

“Tatizo la msongamano ni pana, reli nao wakiwa na huduma nzuri tatizo litapungua, vivyo hivyo kwa upande wa barabara ni mbovu,” alisema meneja huyo wa bandari.

 

Akizungumzia upande wa vifaa, alisema kuwa hivi sasa bandari imenunua vipya, sambamba na kutengeneza nafasi zaidi ya kuhudumia makontena na kujenga ghorofa kwa ajili ya kuhifadhi magari ili nafasi inayotumika kuhifadhi magari itumike kwa ajili ya makontena.

 

Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa muda mrefu sasa kutokana na ucheleweshaji mkubwa wa kutolewa kwa mizigo yao bandarini.

 

Kutokana na hali hiyo ya msongamano wa makontena na meli katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa muda sasa kumekuwapo na taarifa zinazoeleza kuwa baadhi ya meli zimelazimika kusitisha kutoa huduma hapa nchini, hatua ambayo imekuwa ikikanushwa kwa nguvu kubwa na mamlaka za umma nchini.

 

Aidha, taarifa nyingine zimekuwa zikieleza kuwa mlundikano huo wa makontena ambao umekuwa ukiyatia hasara kubwa makampuni ya meli, umesababisha baadhi ya mizigo ya Tanzania kuhofiwa kushushwa katika bandari za nchi jirani na wakati mwingine Mashariki ya Kati.

 

Wakati Mamlaka ya Bandari ikitoa taarifa hiyo, siku chache tu zilizopita TICTS ilitoa taarifa yake kwenye vyombo vya habari ikieleza kuwa, kwa kadiri ilivyozidiwa na uwezo wa kushughulikia makontena, kitengo hicho kilianza kukosa sehemu ya kuhifadhi makontena.

 

TICTS ilizitaja sababu zilizosababisha hali hiyo kuwa ni pamoja na ukuaji wa kuridhisha wa pato la wastani (GDP) katika Tanzania, ambapo wastani wake umekua kwa asilimia 5.8 kwa miaka saba iliyopita.

 

Sababu nyingine ilizozitaja ni kukua kwa kasi ya uchumi wa nchi jirani zisizokuwa na bandari kutokana na kuongezeka kwa biashara, hasa kati yao na nchi za Mashariki ya Kati na nchi za Asia, hasa China.

 

TICTS ilieleza kuwa, kutokana na hali hiyo, upanuzi ulihitajika ili kukabiliana na ongezeko la mizigo hiyo, pia kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inabaki kuwa shindani kwenye biashara hiyo.

 

Kwa mujibu wa taarifa yao, TICTS ilisema kwamba, iwapo uwekezaji zaidi katika nafasi ya nyongeza kwa ajili ya uhifadhi wa makontena katika eneo la kupakulia, pia vifaa zaidi haungefanywa, tija kwenye kitengo cha makontena ingepungua kwa kiasi kikubwa na huenda wateja wangekimbia.

 

Kwa mujibu wa TICTS, hadi mwaka 2007 ilishawekeza dola milioni 15 kwenye vifaa vya kushughulikia makontena pamoja na marekebisho ya miundombinu, kiwango ambacho walidai kilikuwa ni kikubwa kuliko mahitaji yaliyokuwa kwenye mpango wa awali wa uwekezaji.

 

TICTS inadai kuwa iliwasilisha kwa kina mipango ya suluhu ya muda mfupi, ya muda wa kati na mrefu, ikiwa ni pamoja na maendelezo ya kitengo kipya cha makontena, ikionyesha wazi hatari ya msongamano kwa miaka ijayo, isipokuwa kama upanuzi ungefanywa kwa kiwango mwafaka.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents